Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zamu ya Chama kwenda Yanga

Realclatouschama Zamu ya Chama kwenda Yanga

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Julai 2022 winga machachari, Mghana Bernard Morrison alirudi Yanga baada ya kuachwa na klabu ya Simba. Miaka miwili nyuma winga huyo machachari aliikacha Yanga na kujiunga na Simba. Baada ya matukio mbalimbali ya utovu wa nidhamu ya winga huyo, Simba ilimtema na Yanga ikajibebea.

Juni 26, 2023 Simba ilimpa 'Thank You' kiungo wake mkongwe, Jonas Mkude baada ya kudumu klabuni hapo kwa takribani miaka 13. Siku mbili baadaye Yanga ikampitia na kumtangaza rasmi kiungo huyo kwamba ni mali yake.

Kabla ya kuachana na Mkude, Juni 5, 2023, Simba iliachana na winga wake mwingine, Augustine Okrah kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Katika dirisha hili, Desemba 30, 2023 Yanga ilipita na Okrah na kumtangaza kumsajili. Ni katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, ndipo winga huyo raia wa Ghana alipotambulishwa rasmi. Sasa zamu ya Chama.

UMEPIGAJE HAPO? Kiungo Clatous Chota Chama kipenzi cha mashabiki wa Simba anaweza kuvuka upande wa pili na kutua Jangwani. Unajua kwanini? Kuna sababu nyingi.

MOJA. Ni kitendo cha uongozi wa Simba kugawanyika kufanya uamuzi juu ya shauri la nyota huyo wa kimataifa wa Zambia.

Desemba 21, Simba ilitangaza kumsimamisha Chama kwa utovu wa nidhamu sambamba na kiungo mwingine, Nassoro Kapama. Inadaiwa Chama alikaidi kisha akatupiana maneno na kocha wa viungo wa Simba. Hata aliposhauriwa na baadhi ya wachezaji na viongozi wa timu hiyo kuomba radhi kwa kosa hilo, Chama anasemekana aligoma kufanya hivyo.

Hapo ndipo viongozi wa Simba walipoamua kulipeleka suala lake katika Kamati ya Maadili ya Simba iliyopo chini ya uenyekiti wa Kamanda wa Polisi wa zamani, Suleiman Kova.

Tangu suala hilo lifikishwe kwenye kamati hiyo, halijawahi kutatuliwa na baadhi wa wajumbe wa kamati hiyo wakipishana katika kufanya uamuzi juu ya mchezaji huyo.

Baadhi ya wajumbe wanataka timu hiyo yenye masikani yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam iachane na mchezaji huyo kwa kuwa anajiona tayari ameshakuwa mkubwa ndani ya kikosi cha Simba. Wajumbe hao wanaamini Chama anautumia vibaya ufalme wake ndani ya kikosi hicho.

Pia, wapo wajumbe wanaopingana na mawazo hayo na kuifanya kamati kushindwa kufikia muafaka wa suala hilo na wakati mwingine vikao vikishindwa kufanyika.

Inadaiwa uongozi wa Simba, unataka kuachana na mchezaji huyo kutokana na kuiendesha timu hiyo mara kwa mara hususan pale suala lake la usajili linapokaribia. Ikumbukwe aligoma kwenda kwenye kambi ya timu hiyo Uturuki na kuzua taharuki kubwa.

Hofu ya viongozi wa Simba ni kuhofia kumlipa mchezaji huyo gharama kubwa kama watathubutu kuachana na Chama katika dirisha hili la Januari. Lakini kuna uwezekano mkubwa ikaachana naye mwishoni mwa msimu ambapo mkataba wake utakapokuwa umefikia tamati.

MBILI - Sio chaguo la Benchikha Kuna mchezaji mmoja wa kigeni wa Azam FC (jina kapuni) mara aliposikia Simba imemchukua Benchikha kuwa kocha mkuu, akasema mchezaji wa kwanza atakayeondoka Simba atakuwa Chama. Alipoulizwa kwanini akasema muda utaongea na anaamini maneno yake hayawezi kuanguka chini.

Kinachozunguzwa ni kwamba mbali na sakata lake la utovu wa nidhamu, Chama ambaye kwa sasa yuko kwenye kambi ya Timu ya Taifa ya Zambia kwa ajili ya michuano ya AFCON kule Ivory Coast sio chaguo la kocha Abdelhak Benchikha kwasababu haendani na mfumo wake.

Katika mchezo wake wa kwanza wa kimataifa dhidi ya Jwaneng Galaxy kule Eswatini, Benchikha alimwanzisha Chama benchini. Hata dhidi ya Wydad Casablanca ugenini mchezaji huyo alianzia benchini na kuja kuanza katika mchezo wa Dar es Salaam dhidi ya miamba hiyo ya Morocco.

Sio Benchikha tu, Chama hakuwahi kuwa hata chaguo la mtangulizi wa kocha huyo, Roberto Oliveira 'Roberthino' ambaye alithubutu kumtoa uwanjani katika dakika ya 35 dhidi ya Mbeya City na Simba ilishinda 3-2 katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita.

Mara baada ya kumtoa uwanjani, Roberthinho alipata upinzani mkali kutoka kwa mashabiki wakipinga kitendo chake na kumwonyesha kwamba mchezaji huyo hakutakiwa kuguswa. Wengine walithubutu kumwambia kocha huyo kama anaona Chama haingii kwenye mfumo wake, basi yeye kocha anatakiwa kuingia kwenye mfumo wa Chama.

TATU - Nguvu ya Benchika Lakini hali imekuwa tofauti kabisa kwa Benchikha, hakuna shabiki wala kiongozi anayesema chochote kuhusu kumweka benchi Chama. Ni kwasababu kwanza kocha huyo hataki kuona mchezaji anakuwa mkubwa zaidi ya klabu na amepewa nguvu kubwa ya kufanya uamuzi dhidi ya kikosi cha Simba.

Viongozi wanaamini kocha huyo anaweza kukiboresha kikosi hicho kwa kuwaleta wachezaji wanaoweza kuipigania Simba ambayo imepoteza ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu miwili mfululizo iliyopita na haina uhakika wa kuupata msimu huu. Hivyo panga la Benchikha liko kwenye shingo ya Chama.

NNE - Hofu ya kwenda Yanga Viongozi wa Simba hawana hofu tena ya kuogopa kuachana na mchezaji kwa sababu tu atakwenda Yanga. Walikuwa na hofu ya muda mrefu kuhusu Mkude, aliwafanyia vitimbi vingi lakini walihofia kama wangeachana naye angeweza kwenda Yanga, hivyo walimvumilia hadi pale walipoamua liwalo na liwe.

Pia, walichukua uamuzi mgumu wa kuachana na Morrison ingawaje walijua kuwa ni mchezaji mzuri lakini vitendo vyake viliwafanya wafumbe macho na kumwachia huru. Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa Chama. Mwishoni mwa msimu njia itakuwa nyeupe kama atataka kujiunga na Yanga.

Ikumbukwe mara kadhaa Chama alishatajwa kutakiwa na Yanga, Rais wa klabu hiyo, Hersi Said 'Injinia' aliwahi kukaririwa akisema kiungo huyo ni mchezaji mzuri na hakuna timu inayoweza kumkataa kama ikipatikana nafasi ya kumsajili.     WASIKIE WADAU Staa wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba 'Tekelo' amesema endapo Chama akijiunga na Yanga, nje ya ukubwa wa jina lake, atatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuandika rekodi mpya hapa nchini.

Alikiri ni mchezaji mzuri na atabakia kuwa Chama, lakini anapohama, nje ya jina lake, Yanga watataka kuona mchango wake kama aliokuwa nao Simba.

"Tangu zamani mchezaji lazima aipiganie Yanga, kwa maana ya kuonyesha uwezo wake kwanza kabla ya mambo yoyote, jambo la pili kikosi kilichopo hivi sasa, kila mchezaji anaonyesha thamani ya nafasi yake anayocheza, ingawa kama atajiunga nayo kuna chachu itaongezeka kwa wachezaji.

"Kila mchezaji ana kipaji chake, mimi zamani nilikuwa fundi sana wa kupiga mipira ya vichwa, Chama naye ana vitu vyake, ila nasisitiza lazima atafanya kazi ya ziada, sisi mashabiki wa Yanga kama kweli ataachwa Simba tunamkaribisha Jangwani."

Mchezaji mwingine wa zamani wa timu ya Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala alisema mifumo ya makocha inaweza ikamfanya mchezaji imkubali ama imkatae.

"Hakuna ubishi kama Chama kafanya makubwa ndani ya Simba, ingawa kwa sasa kiwango chake kipo chini, huenda mifumo ya makocha waliopita hivi karibuni imemkataa, sasa kama kocha wa Yanga ndiye kampendekeza basi anajua jinsi ya kumtumia ili arejee kwenye kiwango chake," alisema Kasabalala.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live