Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zama mpya Chelsea

Todd Boehly Toddy Boehly

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rasmi zama za bilionea Roman Abramovich kwenye kikosi cha Chelsea zilimalizika mwaka jana, lakini vinasaba vyake bado viliendelea kuishi.

Hata hivyo kadri siku zinavyozidi kwenda vinasaba hivyo vimezidi kuondoka pale darajani na zama mpya za Toddy Boehly zinazidi kushika hatamu.

Wiki hii Chelsea inatazamiwa kumuuza Mason Mount anayehitajika na Manchester United, Kai Havertz anayetakiwa na Arsenal, Kalidou Koulibaly anayetazamiwa kwenda Al Hilal na Cezar Azpilicueta.

Ukimuondoa Koulibaly, ikiwa Mount ataondoka basi kuna uwezekano msimu ujao wachezaji ambao wa zama za Abramovich ambao watabakia watakuwa ni Reece James, Ben Chilwell, Thiago Silva na Kepa Arrizabalaga.

N’Golo Kante tayari ameshatua zake Saudi Arabia kuitumikia Al-Ittihad, Eduoard Mendy naye yupo kwenye hatua za mwisho kutua Al-Ahli.

Baada ya kuondoka kwa mastaa hao zama mpya zinaonekana kuwa ndio zinafuata ambapo Chelsea inaonekana kuwa inajijenga upya.

Chelsea inajijenga kupitia kiazi kipya chini ya Mauricio Pochettino sambamba na wachezaji waliosajiliwa ndani ya miezi 12 tangu Todd Boehly ainunue timu hii.

Pochettino ambaye anatarajiwa kuanza kazi wiki hii atatakiwa kusuka kikosi chake kuanzia golini ambapo atahitaji kipa bora anayeweza kuziba pengo la Eduardo Mendy na inadaiwa kuwa amependekeza jina la kipa wa Inter Milan Andre Onana.

Vilevile eneo la kiungo wa kuziba pengo la N'Golo Kante ambapo jina la kiungo wa Brighton Moses Caicedo ndio linatajwa sana. Tayari upande wa safu ya ushambuliaji kumeshaanza kusukwa ambapo Christopher Nkunku tayari ameshasajiliwa na kuna tetesi zinazodai kwamba wawakilishi wa matajiri hawa wa Jiji la London wapo kwenye mazungumzo na straika wa Inter Milan Lautaro Martinez.

Kwa madirisha mawili yaliyopita kwa msimu uliopita Chelsea ilifanikiwa kuipata huduma ya Enzo Fernandez, Wesley Fofana, Mykhailo Mudryk, Marc Cucurella, Raheem Sterling na Benoit Badiashile ambao walikuwa sehemu ya matumizi ya Pauni 600 milioni ingawa mambo hayakuwa mazuri kwani timu ilimaliza nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Mchezaji mwingine ambaye atajiunga na timu katika dirisha hili anatarajiwa kuwa ni kinda mwenye umri wa miaka 17 Andrey Santos ambaye alisajiliwa katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi kutoka Vasco da Gama kwa Pauni 18 milioni lakini ilishindikana kucheza kwa kuwa alikosa vibali vya kazi.

Ndani ya siku chache zijazo Chelsea itaanza rasmi maandalizi ya msimu ujao na mazoezi yatakuwa yanaongozwa na mtoto wa Pochettino, Sebastiano Pochettino na Jesus Perez ambao watakuwa na kazi yakuwafanyisha wachezaji mazoezi makali ya kuweka miili yao sawa.

Chelsea itasafiri kuelekea Marekani Julai mwaka huu kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu ambapo itaanzia Kaskazini mwa Carolina, Atlanta, Maryland, Philadelphia na Chicago na itacheza mechi za kirafiki dhidi ya Wrexham, Brighton, Newcastle, Fulham and Borussia Dortmund.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live