Baada ya masbishano ya muda mrefu baina ya Haji Manara na Mchambuzi wa Michezo nchini Jemedari Said juu ya Timu gani ya kwanza kufika Nusu Fainali Michuano ya Afrika.
Thabit Zakaria ameamua kuwatolea uvivu na kuwapa somo wawili hao, ambapo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika;
Mwanzo nilidhani watu wapo kwenye utani wao wa kawaida lakini sasa naona kumbe hawajui kabisa, siyo utani.
KUFIKA NUSU FAINALI
CAF wamesema Simba inatafuta nusu fainali ya kwanza ya CAFCL...yaani CAF Champions League au kwa Kiswahili Ligi ya Mabingwa ya CAF.
Ni kweli kwamba Simba haijawahi kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, na siyo tu Simba bali timu yoyote ya Tanzania
Lakini hii ligi ya mabingwa ni mashindano yaliyoanza mwaka 1997 yakichukua nafasi ya mashindano mengine ya Klabu Bingwa Afrika, ambayo yalianza mwaka 1964, yakianzishwa na Rais wa kwanza wa Ghana, hayati Kwame Nkrumah.
Kwenye hayo mashindano ya zamani, yaani Klabu Bingwa Afrika, Simba ilifika nusu fainali mwaka 1974.
Tatizo ni kwamba vyombo vya habari vya Tanzania vimewazoesha walaji wa habari zao kusikia jina la Klabu Bingwa badala ya Ligi ya Mabingwa.
Hiyo imesababisha watu kutojia tofauti ya Ligi ya Mabingwa na Klabu Bingwa.
Klabu bingwa ni mashindano yaliyoemdeshwa kwa mtindo wa mtoano kuanzia mwanzo wa mashindano hadi fainali.
Ligi ya Mabingwa inaenda kwa hatua; mchujo, makundi ambako inachezwa kwa mtindo wa ligi halafu mtoano.
KUSHINDA ROBO FAINALI UGENINI
Wakati Simba wanafika nusu fainali mwaka 1974, walishinda 2-1 ugenini mchezo wa robo fainali dhidi ya Hearts of Oak ya Ghana.
Mabao ya Simba yalifungwa na Adam Sabu (marehemu) na Abdallah Kibaden.
KOMBE LA CAF
Kama ambavyo Kwame Nkrumah alianzisha Klabu Bingwa Afrika, mashindano ya Kombe la CAF ambayo yalianza mwaka 1992, yalianzishwa kwa udhamini wa mfanyabiashara na mwanasiasa kutoka Nigeria, Chief Moshood Abiola.
Haya ndiyo mashindano ambayo Simba ilifika fainali mwaka 1993.
Mashindano haya kama jina lake lilivyo, Kombe la CAF, yalianzishwa maalumu kwa ajili ya timu zilizomaliza nafasi ya pili kwenye ligi za nchi zao.
Wakati huo CAF ilikuwa na mashindano matatu;
Klabu Bingwa Afrika ambayo yalihusisha mabingwa wa ligi za nchi za Afrika.
Kombe la Washindi ambalo lilianza 1975, likishirikisha timu zilizotwaa ubingwa wa Kombe la FA la kila nchi.
Halafu Kombe la CAF kwa ajili ya Washindi wa pili wa ligi.
CAF ilianzisha mashindano haya kuiga mfumo wa UEFA ambao nao walikuwa na mashindano kama haya.