Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera kwenye mtego Coastal Union ni hivi

Zahera X Coastal Tanga Zahera kwenye mtego Coastal Union ni hivi

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Ligi Kuu Bara kumalizika msimu uliopita, mabosi wa Coastal Union waliachana na wachezaji wengi wa kigeni kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kupunguza matumizi kutokana na uchumi wa klabu hiyo.

Dirisha la usajili lililofunguliwa Julai Mosi hadi Agosti 31 mwaka huu, Coastal Union ilibaki na wageni wawili pekee kipa Justine Ndikumana (Burundi) na Mulumba huku wakilenga msimu huu kusajili zaidi wazawa.

Hata hivyo, hadi dirisha la usajili linafungwa, Coastal ilisajili wachezaji wa kigeni wanane ambao ni Beakou Roland (Benin), Djey de Conare (Mali), Shadreck Mulengwe (Zambia), Fran Golubic (Croatia), Henock Mayala (DR Congo), Denis Modzaka (Ghana), Ley Matampi (Congo) na Salah (Ghana), hivyo jumla wamefika wageni 10.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, zinaeleza kuwa kwa asilimia kubwa ya usajili wa wageni sio mapendekezo ya kocha Mwinyi Zahera na kati ya hao wanane kocha ana mapendekezo mawili pekee, Mayala na Matampi.

Chanzo hicho kinasema katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara ambazo timu hiyo imecheza dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji kocha wao bado hakuridhishwa na viwango vya baadhi ya mastaa hao wapya.

“Ni kweli bajeti imekuwa kubwa tofauti na tulivyotarajia, maana bajeti yetu kwenye usajili ilikuwa Sh 100 milioni lakini imezidi kutokana na huu usajili wa wachezaji wapya.

“Tulikubaliana kupunguza kwa asilimia kubwa wageni lakini Coastal ni timu ya wanachama hivyo tunapokea ushauri tofauti ili tufanye vizuri na kuwa kwenye timu nne bora zitakazoshiriki michuano ya CAF hapo mwakani.

“Kocha ameshiriki usajili huu ingawa sio kwa asilimia kubwa maana aliingia kwenye timu wakati tayari tumeanza mchakato wa usajili, wageni hao wamelipiwa gharama za vibali vyote na wadau na wahisani wetu waliowaleta lakini huduma nyingine kama mishahara ni jukumu la klabu,” alisema kiongozi huyo.

Alisema bajeti ya msimu ujao ni Sh 1.3 bilioni ambazo zitapatikana kutoka kwa wadhamini wao ambao ni Azam Tv wanaotoa Sh 40 milioni kwa mwezi, NBC wanatoa Sh20 milioni kwa mwezi, GSM anawapa Sh100 milioni kwa msimu huku wakiweka malengo ya kukusanya mapato ya mechi kwa msimu ya Sh100 milioni.

Kiongozi huyo alisema wamepata udhamini mwingine wa Sh250 milioni kwa mwaka mmoja.

Vibali vilivyolipiwa na wadau wao ni Uhamiaji wanaotoa kibali cha makazi ambacho hutegemea na nchi anayotoka mchezaji ambapo nchi za Afrika Mashariki na Kati ni Dola 1,025 (Sh2.5 milioni), nchi za SADC na Ulaya ni Dola 2,050 (Sh5 milioni).

Kibali cha kufanya kazi kinachotolewa Wizara ya Kazi na Ajira hulipwa Dola 1,000 (Sh2.5 milioni) hii haijalishi mchezaji anatoka nchi gani pamoja na kibali kinachotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Dola 2,000 (Sh5 milioni). Gharama hizo ni kwa kila mchezaji ambapo mchezaji mmoja gharama yake inaweza kufikia Sh15 milioni kwa mwaka.

Msemaji wa klabu hiyo Abbas El Sabri alifafanua; “Ni kweli tulipunguza wachezaji wa kigeni sababu za uchumi. Ila tumepata udhamini na tunataka kumaliza Top 4.”

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: