Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera alia na kina Kagere, Kabunda

Kagere Mk 14 Zahera alia na kina Kagere, Kabunda

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera amegeuka mbogo kwa washambuliaji wa timu hiyo wakiongozwa na Meddie Kagere, Hassan Kabunda na wengineo akiwataka waongeze umakini na ufanisi katika umaliziaji wa nafasi nyingi za mabao zinazotengenezwa kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

Zahera alitoa kauli hiyo jana baada ya kikosi chake kufungwa bao 1-0 na Singida Fountain Gate kawenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa kikiwa ni kichapo cha pili mfululizo baada ya kuchapwa nyumbani mabao 3-1 na Yanga.

Kocha huyo raia wa DR Congo, alisema kwamba katika mechi hizo mbili wachezaji wake wamecheza vizuri, wamepambana na kutengeneza nafasi lakini wanakosa ubora katika kufanya uamuzi wa wapi pa kupeleka pasi za mwisho ili kufunga mabao.

Alisema ukizitoa Simba na Azam ambazo zilitengeneza nafasi 12 na kulifikia lango la Yanga mara nyingi hakuna timu nyingine zaidi ya Namungo iliyofanya hivyo kwani wao walitengeneza nafasi sita, jambo ambalo linaonyesha ana timu nzuri ambayo inaweza kufanya vizuri kama wachezaji wataongeza umakini.

"Leo ambacho nitawalaumu wachezaji wangu ni ubora wa kutoa pasi za mwisho, pasi za kuamua kwa sababu tumepata nafasi nzuri zaidi ya nne lakini hawakuwafanya uamuzi wa kuinufaisha timu lakini wanacheza vizuri, wanapambana na kuleta mpira ila ubora kwenye eneo la mwisho ndiyo tatizo," alisema Zahera.

Katika mchezo wa juzi timu hiyo ilimkosa Meddie Kagere ambaye hakuruhusiwa kwa sababu ametoka Singida Fountain Gate kwa mkopo, Zahera alisema hiyo siyo sababu kubwa ya kikosi chake kuwa butu kwenye umaliziaji.

"Wakati mnasajili wachezaji mnafaa kuwaamini, hata kama Kagere hayupo mchezaji mwingine anaweza kucheza, hatuwezi kusema kwa sababu Kagere hakuwepo ndiyo maana hatukupata nafasi ya kufunga," alisema Zahera na kuongeza;

"Tumecheza mechi nyingine na Kagere akiwamo, tulitengeneza nafasi nyingi na zenyewe hatukufunga, kusema kama Kagere au fulani hayupo hapana, kikubwa ni namna gani mlifika mbele ya goli na tunafika vizuri na wachezaji wanajituma kwa uwezo wao tunakosa kufunga mabao."

Chanzo: Mwanaspoti