Kocha wa zamani wa klabu ya Young Africans Mwinyi Zahera amesema mchezo wa leo Alhamis (Novemba 11) kati ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya DR Congo utakua na vuta ni kuvute kutokana na hesabu za pande hizo mbili.
Taifa Stars itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa ikicheza mchezo wa tano wa Kundi J wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, huku ikikumbukia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo mjini Lubumbashi mwezi Septemba.
Zahera ambaye aliwahi kuwa Kocha Msaidizi wa DR Congo chini ya utawala wa Kocha Florent Ibenge amezungumza na Azam TV kupitia kipindi cha Wednesday Night na kusema: “Ujue mchezo wa kwanza walipokutana ugenini timu ya DR Congo iliwachukulia kawaida Stars na wachezaji ambao walikuwa wanajulikana ni wachache ikiwa ni pamoja na Mbwana Samatta walikuwa wanajua kwamba wachezaji wengi wa Stars ni wa ndani kwa kuwa walishacheza nao watakuja kwa mtindo tofauti.
“DR Congo wanajua kwamba ili waweze kusonga mbele lazima washinde wakifungwa wanatoka katika mashindano na Stars nao wanahitaji kushinda ili kusonga mbele hapo unaona namna gani mchezo utakuwa mgumu kwa timu zote mbili.
“Naweza kusema kwamba hata kama Stars itakuwa ipo Uwanja wa Mkapa basi haimaanishi kwamba watashinda kwa wepesi ni moja ya mchezo mzuri kwa kuwa unazikutanisha timu ambazo zinasaka ushindi.
“Pia hata hao DR Congo nao wameongeza uzito kwenye kikosi na kuwaita wachezaji wenye uzoefu hivyo kila atakayeweza kutumia makosa ya mpinzani atapata ushindi,” alisema Zahera ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa soka la vijana Young Africans.
Taifa Stars inaongoza msimamo wa Kundi J ikiwa na alama 7 sawa na Benin, huku DR Congo ikishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 5 na Madagascar inaburuza mkia kwa kuwa na alama 3.