Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera aanza kulia Polisi Tanzania

Polisi Tz XZahera.jpeg Zahera aanza kulia Polisi Tanzania

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera amekiri kukabiliana na ugumu kwenye kikosi huku akibainisha kupambana na mambo mawili ikiwemo kuinusuru kushuka daraja na ishu ya nidhamu.

Kauli ya Zahera inajiri baada ya kikosi hicho kutoka suluhu juzi dhidi ya Ruvu Shooting na kuzidi kujikita mkiani mwa msimamo huku ikishuhudiwa mshambuliaji wake mpya, Abrahim Hilika akipata kadi nyekundu.

“Ni kweli tuko kwenye kipindi kigumu kwa sababu timu inapigania isishuke daraja ingawa wakati napambana na suala la kupata matokeo chanya pia nidhamu kwa wachezaji inatuangusha jambo ambalo tunabidi kuliangalia,”

“Ukiangalia kuna kadi ambazo mchezaji anapata unaona kabisa ni za kujitakia. Kwa hali ilivyo sasa na jinsi ambavyo tunahitaji kupambana zaidi inabidi kuongeza umakini kuanzia nidhamu kwenye kila mchezo,” alisema.

Katibu Mkuu wa kikosi hicho, Michael Mtebene alisema wana matumaini ya kutoshuka daraja, huku akieleza michezo 11 iliyobaki kumalizia msimu ni ya kufa na kupona.

Kadi nyekundu ya Hilika ni ya nne msimu huu kwenye kikosi hicho baada ya Mohamed Mmanga kupata mbili na Ambrose Awio.

Zahera aliyepewa kuinoa timu hiyo Desemba 2, hajaonja ushindi kwani michezo mitano aliyoiongoza amefungwa mitatu akianza na kichapo cha bao 1-0 kwa Azam, 3-0 kutoka na Yanga na 2-0 dhidi ya KMC, huku miwili akiambulia sare ya kufungana mabao 3-3 na Coastal Union kisha suluhu na Ruvu Shooting.

Chanzo: Mwanaspoti