Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera aanika ramani ya ushindi

80974 Zahera+pic Zahera aanika ramani ya ushindi

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

KIKOSI cha Yanga kimeondoka alfajiri ya leo kwenda jijini Mwanza, huku wakiwa kwenye mkakati mzito kuelekea maandalizi ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao, lakini akili zote za mabosi wao zipo katika pambano la kimataifa watakapowakaribisha Pyramids ya Misri.

Yanga itaialika Pyramids kwenye mchezo wao wa kwanza wa mtoano ‘playoff’ wiki ijayo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kabla ya kurudiana nao wiki moja baadaye ili kuamua hatima yao ya kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Misimu ya 2016 na 2018 Yanga ilifanikiwa kuvuka hatua kama hii na kucheza makundi ikiwa timu pekee ya Tanzania kufanya hivyo katika michuano hiyo ya pili kwa ngazi za klabu baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa ambayo pia walishiriki 1998.

Kutokana na uzito wa mchezo huo utakaoiweka Yanga kwenye matawi ya juu kama itavuka salama hatua hiyo, mabosi wa klabu hiyo kwa sasa wanachofanya ni vikao vizito, lakini pia wamepokea mkakati mzito kutoka kwa kocha wao Mwinyi Zahera aliyerejea nchini juzi alfajiri akitokea Ufaransa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo amesema Zahera ameanika ramani ya ushindi kwa timu hiyo na kutaka afanyiwe mambo matatu muhimu ili kazi yake iwe nyepesi.

Gumbo ameyataja mambo hayo matatu katika maandalizi ikiwamo kuikubali kambi ya timu kuwa jijini Mwanza kisha mchezo kufanyika jijini hapo, lakini akitaka kambi yao kuwa mbali na mjini ili kuwapa utulivu vijana wake.

Pia Soma

Advertisement
“Kocha anataka kambi iwe Mwanza hilo, halina ubishi sasa ila kitu anachotaka ni kuhakikisha inakuwa mbali na mji ili kuwe na utulivu kuwawezesha wachezaji kuongeza umakini,” alisema.

Gumbo alisema jambo la pili ambalo Zahera ametaka ni kambi yao kuwa na huduma nzuri zaidi ambapo yapo maelekezo ambayo ameyataka katika mfumo wa chakula.

“Kuna maelekezo ambayo yapo katika malazi na huduma zote sahihi ambazo anataka zifanyiwe marekebisho kwa kuboreshwa zaidi kuliko tunachofanya sasa.

Alitaja jambo la tatu ni kupatikana kwa taarifa zote za ufundi na ubora wa mikanda ya Pyramids ambayo tayari imeshaanza kufanyiwa kazi.

“Utafutwaji wa taarifa za hawa jamaa pia ni kitu ambacho amekihitaji na hilo tayari limeshaanza kufanyiwa kazi, nafikiri baada ya mechi ya Mbao tutakuwa na hayo yote aliyoyahitaji,” alisisitiza kigogo huyo.

Lengo la Zahera ni kutaka kuwasoma wapinzani wao hao ili kujua ubora na udhaifu wao na namna ya kuwadhibiti kwenye mechi hizo za kuwania makundi ya shirikisho.

Pyramids inayoshiriki michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza katika mechi zao nne za raundi ya awali na ya kwanza walishinda jumla ya mabao 5-1 dhidi ya Etoile du Congo ya Congo Brazzaville na 2-1 mbele ya CR Belouizdad ya Algeria.

Juzi timu hiyo ilikuwa uwanjani nyumbani kwenye Ligi Kuu ya Misri na kubanwa mbavu na Smouha kwa kutoka suluhu na Jumatatu itarudi tena dimbani kuvaana na El Entag El Harby ugenini katika mfululizo wa ligi hiyo wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo na alama zao nane baada ya mechi nne, nyuma ya vinara Al Ahly.

MSIMBAZI WATAJWA

Wakati uongozi ukipanga yao na kocha wao, Gumbo alidokeza pia kwenye vikao vyao na makundi ya wanachama wamesisitiza wanataka kuona uongozi wao wanafanya maandalizi ya mchezo huo wa kimataifa kwa kiwango kama kile kinachofanywa wanapokuwa wanajiandaa kukabiliana na watani wao wa Simba.

Wanachama walisema wanaamini maandalizi yakiwekwa kwa kiwango cha kuwakabili Simba inaweza kuwafanya wapate matokeo mazuri, hata kama wapinzani wao wanaoonekana kuwa wazuri wachezapo ugenini.

“Wanachama wanataka kuona maandalizi yanakuwa ya kiasi kikubwa kama tunavyojiandaa kucheza na Simba. Kama uongozi tumeyachukua hayo, japo nasi tupo katika kiwango kikubwa kuelekea mechi hiyo, lakini nao wametuambia wako katika maandalizi hayohayo kwa ajili ya kuhakikisha Mwarabu anakufa huku ugenini,” alisisitiza.

Chanzo: mwananchi.co.tz