Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zabona: Bodaboda zilivyomnyima ulaji Yanga, Simba

Zabona Zabona: Bodaboda zilivyomnyima ulaji Yanga, Simba

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

‘Namwachia Mungu’. Ni kauli ya staa na kipenzi cha mashabiki wa Tanzania Prisons, Zabona Hamis akielezea sintofahamu inayomkumba pale alipopata ofa za Simba na Yanga.

Winga huyo ambaye kwa sasa ndiye injini ya Prisons, amefunguka mengi kuelezea misukosuko inayompata ndani na nje ya uwanja, siri ya ubora wake na pacha yake dhidi ya Samson Mbangula.

Pia nyota huyo wa zamani wa Alliance, Lipuli na Fountain Gate ameeleza ndoto yake ya kuvaa gwanda ambayo kwa sasa imebaki mikononi mwa mmiliki wa shule aliyosoma kumpatia vyeti vyake aweze kukamilisha mchongo huo.

AJALI ZA PIKIPIKI

Zabona aliyelelewa na Akademi ya Alliance ya jijini Mwanza anasema bado hajaelewa kinachomtokea pale inapotokea kupata ofa za kujiunga na miamba ya soka nchini, Yanga na Simba.

Anasema akiwa Alliance FC wakati timu hiyo ikishuka daraja msimu wa 2019/20 alipata dili la kujiunga na Yanga na baada ya kusaini mkataba wa awali na kwenda nyumbani kwao, Buchosa mkoani Mwanza aligongwa na pikipiki.

Anasema baada ya ajali hiyo alijikuta nje ya uwanja kwa takribani misimu miwili kisha kuanza kuhangaika kupata timu ya kuchezea hadi kuibukia Lipuli aliyodumu kwa nusu msimu ikiwa Daraja la Kwanza (Championship) msimu wa 2021/22. Anaongeza baadaye alirejea tena Alliance FC iliyokuwa Daraja la

Kwanza na kumaliza nao msimu huo akitokea Lipuli ambayo hakuambulia hata senti moja katika muda wa miezi minne aliyohudumu pale.

“Yanga nilikuwa nimesaini mkataba wa awali, hivyo nikaenda nyumbani Buchosa kwa mapumziko, lakini nikiwa kwenye harakati za kitaa niligongwa na pikipiki.”

“Ajali hiyo iliniweka nje kama misimu miwili, hivyo dili hilo likapotea, nikaanza kujitafuta upya hadi kuibukia Lipuli kabla ya kurejea tena Alliance kipindi hicho zikiwa Daraja la Kwanza,” anasema Zabona.

Anasema baadaye alijiunga na Fountain Gate ya Championship kabla ya kusaini Tanzania Prisons ambayo alikuja kujaribu bahati na kujikuta akila mkataba wa miaka mitatu hadi sasa.

Anaeleza msimu uliopita akiwa na Tanzania Prisons baada ya mchezo wao dhidi ya Simba walipolizwa mabao 7-1, viongozi wa Wekundu walimpigia simu wakiihitaji huduma yake.

Anasema baada ya mazungumzo na vigogo hao, aliwaunganisha na mabosi wa Prisons ili kumalizana mezani lakini kilichomkuta ni sawa na kile cha Yanga.

“Baada ya kuzungumza nao walihitaji Prisons watume mkataba wa mshahara wangu ili waone namna ya kuvunja ili niende Simba, lakini nikiwa katika mishe zangu navuka barabara pale Magereza karibu na kambini niligongwa na pikipiki.”

“Ajali hiyo manusura initoe uhai kwa kuwa nilipopelekwa Hospitali ya Kanda Mbeya haikuwezekana kutokana na damu kuwa karibu na ubongo, ndio nikasafirishwa kwa ndege hadi Muhimbili.”

“Nashukuru uongozi wa Prisons walikuwa bega kwa bega na mimi hadi kuwa nje kwa takribani msimu mzima na ofa hiyo kuishia hewani,” anasema Zabona.

Nyota huyo anaeleza kila kitu kina mipango yake, hivyo yeye amemwachia Mungu ambaye alimleta duniani, hivyo muda wake ukifika ndiye atajua atakuwa wapi na katika mazingira gani.

AKESHA STENDI KUU MBEYA

Utafutaji wa maisha una siri kubwa kwa kila mtu, ndivyo ilivyokuwa kwa staa huyo wakati akijiunga na Tanzania Prisons hadi kufika kukesha kituo cha mabasi jijini Mbeya.

Nyota huyo ambaye amekuwa na kiwango bora msimu huu, anasema wakati anajiunga na Maafande hao alienda kujaribu bahati na baadaye kufanikiwa kupata saini chini ya aliyekuwa kocha wao, Patrick Odhiambo raia wa Kenya.

“Wakati natoka Fountain Gate Dodoma nilikuwa na nauli tu na baada ya kufika Mbeya nilibakiwa na Sh1,600 nikajikuta nalala stendi kuu hadi alfajiri ili niende Prisons kufanya majaribio.”

“Nilijiuliza nikimpigia Kocha Odhiambo alfajiri saa 10 tena kwa shida zangu haitakuwa vizuri hivyo nikaamua nikeshe na wenzangu tunaangalia runinga pale stendi hadi kupambazuke.”

“Nashukuru nilipofika Prisons mazoezi ya siku tatu tu walinikubali hadi kusaini miaka mitatu nikiwa na Edwine Balua na kipa Mussa Mbisa japokuwa wao walikuwa tayari wameshasaini,” anasema Zabona.

ANASOTA NA VYETI

Nyota huyo anasema wakati akiendelea kuutumikia mkataba wake, bado hajafunga milango kwa timu nyingine itakayohitaji huduma yake iwapo itafuata utaratibu.

Hata hivyo, anafafanua malengo yake ni kupata ajira ya Jeshi la Magereza japokuwa kwa sasa ishu ya kupata vyeti vyake shule aliposomea imekuwa changamoto.

Anasema pamoja na mazungumzo ya mara kwa mara ya mmliki wa shule hiyo (jina tunalo) iliyopo jijini Mwanza kumwomba alipie kidogo kidogo hadi kukamilisha Sh30 milioni alizomtaka alipe lakini bado hajaridhia.

“Mimi nilienda pale shuleni kwa vipaji maalumu, hivyo kaniambia nilipe Sh30 milioni nipate vyeti na nimekubali anipe cheti ili niwe nalipa kwa awamu baada ya ajira.”

“Nilimhakikishia nipo tayari kuandikiana barua mbele ya wanasheria hadi nyumbani, walikubali kutoa eneo la shamba lakini bado hajaridhia, naendelea kusubiri kwani nia yangu nipate ajira,” anasema.

AFICHUA SIRI NA MBANGULA

Staa huyo ambaye amekuwa moto kwa sasa, anasema anafarijika zaidi kwa muunganiko wake na straika wa timu hiyo, Samson Mbangula ambaye wamekuwa na pacha nzuri. Anasema wamekuwa na mafanikio mazuri kutokana na muunganiko wa timu baada ya kuelewa falsafa ya kocha mpya Ahmad Ally aliyeingia kuchukua nafasi ya Fredi Felix ‘Minziro’.

“Napenda sana nikiwa na Mbangula japokuwa hata yeyote naweza kucheza naye kama atafuata mfumo wa kocha, mimi naweza kucheza mazingira yoyote lakini kufunga na kutengeneza bao,” anasema nyota huyo.

Anasema kwa sasa anafurahishwa na matokeo waliyonayo tofauti na walivyoanza akieleza ushirikiano wa timu ndiyo siri ya mafanikio yao.

“Binafsi nashukuru kwa mashabiki kutambua uwezo na mchango wangu kikosini, lakini lazima wajue soka ni ushirikiano, hakuna mchezaji anayeweza kutoka golini hadi golini akafunga bao,” anasema Winga huyo.

Chanzo: Mwanaspoti