Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yusuph Dabo: Nauona ubingwa Azam FC

Yousuf Dabo Azammm Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindi wa mabao 2-1 ilioupata mbele ya Geita Gold, umempa jeuri kocha mkuu wa Azam, Youssouph Dabo kiasi cha kutamka sasa anaiona nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, licha ya kukiri upinzani mkubwa dhidi ya Simba na Yanga.

Azam ilipata ushindi huo uliokuwa wa 11 msimu huu katika mechi ya 15 za duru la kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi 35, moja pungufu na ilizonazo Simba inayoshika nafasi ya pili na nane pungufu kwa ilizonazo Yanga kileleni.

Mabao ya Azam yaliwekwa kimiani na Gibril Sillah na Idd Seleman ‘Nado’ na kuwafanya kila mmoja kufikisha manne, huku lile la kufutia machozi la Geita likifungwa Tariq Seif likiwa ni la tatu kwake katika ligi hiyo.

Akizungumzia mchezo huo, Dabo alisema ushindani umekuwa mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu hivyo jambo kubwa kwao ni pointi tatu zilizowaweka katika hali nzuri ya kiushindani.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kwa sababu tuna pengo la pointi na walio juu yetu ingawa tuko kwenye mstari mzuri. Nafurahishwa kwa kiasi kikubwa na aina ya upambanaji unaoonyeshwa na wachezaji kuanzia mwanzo hadi mwisho,” alisema.

Dabo aliongeza, siri kubwa ya kufanya vizuri ni maelewano mazuri aliyonayo kwa wachezaji na viongozi ila amewataka kuendelea kupambana zaidi kwani kasi ya wapinzani wao sio ndogo hivyo jitihada kubwa zinahitajika kila mchezo.

“Mchezo mmoja unabadilisha taswira nzima na hicho ndicho kitu kimetutokea kwa sababu tulikuwa tunaongoza kwa muda mrefu lakini baada ya wenzetu kucheza michezo ya viporo wamesogea juu. Hii ni ishara ya kutobweteka tulipo.”

Mara ya mwisho kwa Azam kutwaa ubingwa wa Bara ilikuwa msimu wa 2013-2014 ilipoivua Yanga kwa kubeba bila kupoteza ikikusanya pointi 62 ikiifikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Simba msimu wa 2009-2010 na kwa msimu huu katika mechi 15 ilizocheza, imeshinda 11, sare mbili na kupoteza mbili huku ikifunga mabao 38 na kufungwa 12.

Chanzo: Mwanaspoti