Siku moja baada ya kumalizika kwa msimu wa 2021/22, Yusuf Bakhresa, mmoja wa wakurugenzi wa Azam FC alitangaza vita kwenye mbio za ubingwa katika msimu unaofuata, 2022/23.
Majina ya wachezaji wenye hadhi kubwa pamoja na wataalamu kwenye benchi la ufundi wakashushwa Chamazi kwa mbwembwe kubwa.
Mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Kally Ongala ambaye pia aliwahi kuwa kocha msaidizi katika msimu ambao Azam FC walishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara akatangazwa kuwa kocha wa washambuliaji.
Azam FC ikawa timu ya kwanza Tanzania kuajiri kocha maalumu kwa ajili ya washambuliaji tu.
Yusuf akawa anajenga timu na nchi ikaingia hofu. Mashabiki wa Azam FC wakaona ligi inachelewa kuanza. Lakini kwa watu tunaoifahamu Azam FC kiundani zaidi hilo lilikuwa kosa la kwanza la Yusuf Bakhresa.
Kally Ongala ni rafiki wa karibu sana wa Yusuf miaka na mikaka. Yeye ndiye aliyemrudisha kutoka Sweden mwaka 2010 aje kuitumikia Azam FC. Na alipostaafu baada ya msimu wa 2010/11, Kally akawa sehemu ya benchi la ufundi chini ya Stewart Hall.
Hall na Kally walielewana sana, lakini baada ya fainali ya Kombe la Kagame 2012, Hall akafukuzwa Azam FC, Kally akabaki. Akaja kocha mkuu wa kuitwa Boris Bunjak, lakini huyu jamaa hakuiva na Kally. Maisha yake yakawa mafupi sana Chamazi.
Akarudi Hall lakini akaondoka tena mwaka 2013 baada ya mechi ya kihistoria ya 3-3 dhidi ya Mbeya City. Badala yake akaja Joseph Marius Omog na akaisaidia Azam FC kushinda ubingwa.
Ulipoanza msimu mpya wa kutetea ubingwa, mambo yakawa magumu. Azam FC ambayo ilikuwa na mechi 38 bila kupoteza ikafungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu pale Chamazi na dhidi ya Ndanda FC kule Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Benchi la ufundi likalalamika kwamba Kally haendi nao pamoja yaani hawaimbi wimbo mmoja, basi akatolewa kafara na kuondoka Azam FC. Kitendo hiki kilimchefua sana Yusuf, na akataka kuwaondoa wote waliokuwa sehemu ya benchi kumlipia rafiki yake Kally kisasi.
Kukawa na mvutano kati yake na wakurugenzi wenzake ambao ni kaka zake. Wenzake wanataka waliobaki kwenye benchi waendelee kuwepo, yeye akitaka waondoke. Akawazidi nguvu na ndipo alipoondoka Omog, Ibrahim Shikanda na hata Patrick Kahemele ambaye alikuwa meneja wa timu.
Yusuf akashinda vita ya kumlipia kisasi rafiki yake Kally. Yusuf na Kally urafiki wao ni zaidi ya undugu...wanaiva sana. Kuna wakati Yusuf alikuwa akiishi Uingereza ambako Kally ndiyo nyumbani kwao upande wa mama. Akawa Digala wake. Kwa hiyo anamuaminia sana. Ukitaka kumkera Yusuf mguse Kally wake.
Kwa hiyo alipomleta tena Azam FC kama kocha wa washambuliaji ilikuwa ku changanya kazi na urafiki. Haukuwa uamuzi sahihi hata kidogo. Kina Abdihamid Moallin hawakufurahishwa na kazi ya Kally na walipojaribu kufanya wajuavyo kwa maslahi ya timu wakaondoka!
Yusuf akataka Kally akabidhiwe timu, lakini wakurugenzi wenzake ambao ni kaka zake wakakataa.
Timu ikawa chini ya Mohamed Badru, Kally akawa msaidizi. Chini ya Badru timu ilicheza mechi moja tu, ile sare ya 2-2 dhidi ya Yanga. Hii inabaki kuwa mechi bora zaidi ya Ligi Kuu msimu huu.
Akaletwa kocha mpya, Denis Lavagne kutoka Ufaransa. Yusuf hakutaka kocha mpya alitaka Badru na Kally waendelee, akihofu kocha mpya anaweza kuja kumkataa Kally wake. Lakini nguvu ya wakurugenzi wenzake ikamzidi na ndipo aliposhuka Lavagne.
Lakini ujio wa kocha huyu ulikuwa moto kwa wengine wote waliohusika na kuja kwake, ukiacha wale wakurugenzi. Alikuwa akiwakemea kwa kila jambo linalotokea kwenye timu...’kocha wenu huyo’.
Hakuchukua raundi, Lavagne akaondoka. Hapohapo Yusuf hakusubiri wakurugenzi wenzake waseme kitu akatangaza kwamba Kally akachukua timu kwa muda. Bahati nzuri upepo ukawa upande wake na Azam ikashinda mechi nane mfululizo.
Hii ilimpa jeuri kubwa sana Yusuf mbele ya wakurugenzi wenzake, ‘mnamuona Kally wangu?’
Kumuunga mkono, akaongeza bonasi ya ushindi kwa zaidi ya mara 10. Lakini kikanuni kaimu kocha mkuu hukaa benchi kwa mechi tano tu. Mechi ya tano ya Kally ilikuwa dhidi ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.
Yusuf akataka Kally aendelee, wenzake wakataka aletwe kocha mwingine. Hata hivyo, wakurugenzi wote lengo lao lilikuwa timu ishinde. Kwa kuwa timu ilikuwa inashinda chini ya Kally, basi wakaacha maisha yaendelee.
Lakini Kally hana vyeti vya kumfanya awe kocha mkuu wala kocha msaidizi. Ndipo vyeti vya kocha wa makipa, Danny Cadena vikapelekwa TFF kusajiliwa kama kocha mkuu. TFF wanajua Cadena ndiye kocha mkuu lakini kwenye uwanja wa mazoezi, Kally ndiye kocha.
Hata hivyo Cadena kama kocha anayejua thamani yake haridhishwi na ufundishaji wa Kally, anaona kama ataharibu cheti chake. Hilo nalo limeshamjengea chuki na wakati wowote tutasikia breaking news kutoka Chamazi au itapita kimyakimya kama ya Mhispaniola mwenzake Mikel Guillen, lakini anaweza asimalize msimu!
Kila mtu klabuni anajua kwamba Kally hatoshi kuwa kocha mkuu wa Azam FC, lakini anaogopa kusema asije akamkera bosi. Wakati Yusuf anatumia pesa nyingi kuijenga Azam FC, pia anatumia nguvu nyingi kuibomoa.