Yeye anaamini adui yake namba moja kabla ya mpira ni mpinzani anayeelekea kuivamia safu yake ya ulinzi.
Huyu ndie kiungo ambae mpaka leo anaishi uhalisia wa ile kauli, 'Mpira uende mtu abaki'. Kwake ni dhambi kubwa kumuacha mpinzani akatize katika eneo lake salama hata kama nyuma yake ana walinzi wa kuzuia hatari.
Ndiyo maana haishtui kusikia ameingia katika kitabu cha mwamuzi zaidi ya mara 80. Aliwahi kusema uwanjani ana rafiki mmoja tu, Sergio Ramos. Na hiyo ni kwasababu Ramos humpongeza katika matukio ambayo wengine humlalamikia.
Kwa waliomfuatilia Ramos vizuri watakuwa wanafahamu ni matukio gani huyafurahia zaidi kiwanjani. Kwa Sergio Ramos, ni aibu mno kwa beki kutokuogopwa na mshambuliaji.
Ndiyo maana hata Mourinho alipoambiwa achague wachezaji wawili anaodhani wanamfaa zaidi katika kikosi cha Real Madrid, yeye alimuacha Ronaldo na Benzema akawachagua Casemiro na Ramos.
Mourinho na yeye ana imani zake, kwamba ili ushinde mechi ya mpira unahitaji wanaume wa shoka. Wapo wapi wengine zaidi ya Casemiro na swahiba wake??
Jana kabla mchezo, timu ya ufundi ya Manchester United ilitumia muda mwingi kumkumbusha Casemiro juu ya mechi ijayo dhidi ya Arsenal hivyo ajitahidi kadiri awezavyo kukiepuka kitabu cha mwamuzi. Kadi moja ya njano ingemkosesha mechi ya Arsenal.
Lakini maji hayasahau baridi! Alivumilia kwa dakika 80 kisha Zaha alikatiza mbele yake. Ikawa hadithi ya binadamu aliyeingia katika msitu wa mazimwi. Casemiro akafanya kile anachokifanya bora mara zote. Uvunguni, ni foul na hayupo mechi ijayo. Rahisi sana.
'Role model' wake ni Zidane Zinedine. Na hiyo ni kwa sababu Zizzou hakuwa mtu wa masikhara uwanjani, si kwa sababu ya ufundi wake. Yeye anawahusudu watu wa shoka. Yeye anamuhusudu Gilberto Silva na Captain Dunga.
Huyo ndie Casemiro halisi anayeamini dakika tisini za mpira uwanjani ni vita na mpinzani anayelishambulia lango lake ni Simba anayetaka kula watoto wake.
Mimi mwenyewe namuhusudu sana