Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema ubora wa Luis Miquissone na Aubin Kramo unamuongezea upana wa kikosi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa na African Super League.
Robertinho amefunguka hayo baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Cosmopolitan mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, huku kipa mpya wa timu hiyo, Ayoub Lakred akianza kwa kuruhusu bao.
Simba iliibuka na ushindani huo ikichezesha wachezaji wote wa kikosi cha kwanza kwa asilimia kubwa, huku Miquissone akitumika kwa dakika 90 za mchezo akionyesha kiwango cha juu.
“Nimetoa nafasi kwa wachezaji wote ili kupata nafasi ya kuona uwezo wa kila mmoja. Nafurahi kuona Miquissone ameanza kuonyesha uwezo mzuri kama leo nimempa dakika zote na ameonyesha kiwango bora.
“Kwa upande wa Kramo licha ya kuingia kipindi cha pili kwenye mechi zote mbili za kirafiki, pia amenipa kitu kikubwa akifunga mabao mawili. Nitaendelea kumpa nafasi zaidi ili aweze kuwa bora zaidi ya alipo sasa,” alisema.
Robertinho alisema Kramo ni mchezaji mzuri na ana uzoefu mkubwa kutokana na kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, ingawa anamtengeneza ili azoea ligi ya Bara.
“Ni mchezaji mzuri lakini bado naendelea kumpa muda zaidi ili apate uzoefu wa ligi ya Tanzania. Tayari nimeanza kumpa dakika chache kwenye mechi za kirafiki na ameonyesha uwezo mkubwa kwani ni miongoni mwa wachezaji watakaocheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na naamini watatusaidia,” alisema.
Mabao ya Simba kwenye mchezo na Cosmopolitan yalifungwa na Moses Phiri, Jean Baleke, Willy Onana, Kramo na Shaban Chilunda, huku bao la wapinzani wao likifungwa na Mohammed Samatta kwa mkwaju wa penati baada ya Shomari Kapombe kushika mpira ndani ya eneo la hatari.