Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Youssouph Dabo anakuja Tanzania Je, ni timu gani?

Youspppp Youssouph Dabo anakuja Tanzania Je, ni timu gani?

Wed, 26 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa 2020/21, klabu changa ya Tenguteh FC ya Senegal ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwashangaza Raja Casablanca kwenye raundi ya kwanza.

Mchezo wa kwanza uliofanyika Senegal ulimalizika kwa sare ya 0-0 na Raja wakajua watakwenda kumalizia kazi nyumbani Morocco.

Kuonyesha kujiamini, wakawapa lifti wapinzani wao kwenye dege lao kubwa waliloenda nalo ugenini. Lakini kwa mshangao wa wengi, Tengueth wakaenda kukomaa mjini Casablanca na mechi ikaisha tena kwa suluhu, hivyo kuamuliwa kwa mikwaju ya penati. Wakashinda maao 3-1 na Raja wakiwa nyumbani wakatolewa.

Kikosi cha Tengueth kilikuwa na nyota kama Pape Sakho wa Simba na Malikcou Ndoye wa Azam ambaye alikuwa nahodha.

Lakini aliyetengeneza mchoro wa ramani ya maangamizi kwa Raja alikuwa kocha wao, Youssouph Dabo.

Baada ya msimu huo, Sakho akaja Tanzania kujiunga na Simba, Dabo akaenda kwenye klabu kubwa kuliko zote nchini Senegal, ASC Jaraaf de Dakar.

Lakini, Aprili 10, mwaka huu, klabu hiyo ikatoa taarifa kwamba Dabo ameachia ngazi kwa makubaliano ya pande mbili kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya.

Baada ya taarifa hii Dabo mwenyewe akaibuka na kuishangaa klabu kwa kutoa taarifa yenye kupotosha. Akasema yeye alishaachana na klabu hiyo tangu mwanzoni mwa Februari mwaka huu na tangu hapo timu iko chini ya aliyekuwa msaidizi wake.

Akasema kisa cha kufikia makubaliano ya kuachana na klabu hiyo ni kauli yake mbele ya bodi kwamba msimu ujao atakwenda Tanzania.

Bodi haikufurahishwa, hivyo badala ya kusubiri hadi msimu uishe wakaona bora tu aondoke mapema - akaondoka kwa makubaliano ya pande mbili.

Lakini anashangaa kuona taarifa wanaitoa sasa katika kipindi ambacho klabu haifanyi vizuri, ilhali makubaliano yalifanyika tangu Februari.

Ni kauli hiyo ya MSIMU UJAO NAENDA TANZANIA ndiyo inayochagiza andiko hili. Dabo anakuja Tanzania msimu ujao, je ni klabu gani?

Kocha wa kiwango cha Dabo anatarajiwa kuhudumu kwenye timu za hadi ya juu kama Yanga, Simba, Azam, Taifa Stars na labda kidogo Singida Big Stars.

Timu zingine chini ya hapo ni vigumu kuweza kummudu, lakini lolote linaweza kutokea. Yanga kwa sasa wako na Nabi na Kaze ni vigumu kuwaza kwamba wanaweza kuhitaji kocha msimu ujao.

Simba wako na Robertinho na Mgunda, ni vigumu kuwaza hivyo pia. Taifa Stars wako na Amrouche nao ni vigumu, hasa ukizingatia ni kocha mpya bado.

Singida Big Star wako na babu Hans, nao ni vigumu kuwawazia kutaka kocha mpya. Azam iko na Kally, japo kwenye makabrasha ya TFF linasomeka jina la Cadena.

Yawezekana kabisa Dabo msimu ujao akawa Chamazi, na hata tetesi nchini Senegal zinadai hivyo. Kwa mujibu wa mwandishi maarufu wa Senegal, Saikou Seydi, Dabo atajiunga na klabu ya Azam ya Dar es Salaam.

Mwandishi huyo aliandika hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, mara tu baada ya klabu ya Jaraaf kutoa taarifa. Kama ni kweli Dabo atatua Azam basi ataungana na nahodha wake Malickou Ndoye ambaye alianza vizuri nchini, lakini baada ya kuumia na kukaa nje miezi mitatu hajarudi vizuri kama alivyoanza.

DABO NI NANI?

Jina lake kamili ni Youssouph Dabo. Alizaliwa Novemba 11, 1979 mjini Sagatta nchini Senegal. Kwa sasa ana miaka 43.

Alicheza soka nchini mwake kisha Tunisia na baadaye Ufaransa ambako alicheza madaraja ya chini. Alipostaafu akasomea ukocha na akaanza rasmi mwaka 2012.

BAADHI YA MAFANIKIO

Yafuatayo ni baadhi ya mafanikio yake kama kocha. Mwaka 2016, akiwa na Tengueth alishinda ubingwa wa Kombe la Ligi.

Mwaka 2017 akiwa kocha wa Tengueth alifika fainali ya Kombe la Senegal (sawa na Kombe la Shirikisho la Azam hapa nchini)

Desemba, 2018 alitwaa ubingwa wa vijana chini ya miaka 20 kwa timu za taifa ukanda B wa Afrika Magharibi (Wafu B), mashindano yalipofanyika Togo.

Februari 2019 alichaguliwa kuwa kocha bora wa Afcon chini ya miaka 20 huko Niger alipoisaidia Senegal kufika fainali. Juni 2019 aliiongoza Senegal kufika robo fainali ya Kombe la Dunia chini ya miaka 20 nchini Poland.

Julai 2019 alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu ya taifa ya Senegal iliyofika fainali ya Afcon kule Misri. Agosti 2019 akiwa kocha wa timu ya taifa ya Senegal chini ya miaka 23, aliiongoza kushika nafasi ya tatu na kushinda medali ya shaba kwenye michezo ya Afrika jijini Rabat, Morocco.

Desemba 2019 aliiongoza Senegal kushinda ubingwa wa kanda ya Wafu mashindano yaliyofanyika Guinea. Machi 2020 aliiongoza Senegal kushinda ubingwa vijana chini ya miaka 20 wa mashindano ya mataifa ya Kiarabu. Senegal ilishiriki kama wageni waalikwa mashindano yaliyofanyika Saudi Arabia.

Novemba 2020 akiwa kocha wa timu ya taifa ya Senegal chini ya miaka 20 walifika fainali kuwania ubingwa wa kanda A ya Afrika Magharibi. Msimu wa 2020/21 alishinda ubingwa wa ligi ya Senegal akiwa na Tengueth.

Kwa mujibu wa wasifu huu, asilimia kubwa ya maisha ya ukocha ameyaishi akiwa na timu za vijana akija Tanzania kufundisha timu kubwa, atamudu?

Chanzo: Mwanaspoti