Alama Nane ambazo wamewaacha Watani zao wa Jadi Simba SC, zinaendelea kuwapa Jeuri Mabingwa Watetezi wa Tanzania Bara Young Africans kufanya vizuri kwenye michezo ijayo ya Ligi Kuu na kutetea taji lao.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Young Africans inayonolewa na Kocha Mkuu kutoka nchini Tunisia Nasreddine Nabi, ipo nafasi ya kwanza ikiwa na alama 62, huku Simba SC ikiwa nafasi ya pili na alma 54, zote zikiwa zimecheza michezo 23.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema dhumuni lao ni kuendelea kupambana na kushinda michezo iliyobaki, ili kufanikisha lengo la kutetea Taji la Tanzania Bara msimu huu 2022/23.
Amesema wanatambua Ligi Kuu ina ushindani mkubwa, hivyo Benchi la Ufundi kwa kushirikiana na Uongozi wanaendelea kupambana ,ili kuhakikisha hawaangushi alama yoyote katika kipindi hiki cha kuelekea ukingoni mwa msimu huu.
“Ni alama nyingi ambazo tumewaacha wale wanaotufuata, bado tuna michezo mbele yetu, tutapambana kushinda zote ili kutetea taji letu.
“Kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya kupambania mataji ambayo tunatetea ikiwa ni pamoja na ligi, hili ni muhimu kwetu ukizingatia tunaongoza katika msimamo, tunaamini kwamba tutafikia malengo yetu,” amesema Ally Kamwe
Young Africans itashuka Dimbani Azam Complex-Chamazi keshokutwa Jumapili (Machi 12), kuikabili Geita Gold FC inayoshika nafasi ya tano katika Msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 34.