Mkuu wa Benchi la Ufundi la Young Africans, Nasreddine Nabi ametoa mapumziko ya siku moja sawa na saa 24 kwa wachezaji wake wote pamoja na mfungaji wa mabao mawili dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria.
Young Africans juzi Jumapili (April 23) ilifanikiwa kuifunga Rivers United mabao 2-0 yote yakifungwa na Mayele katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Jumapili (April 30) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar saa moja kamili usiku.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, mara baada ya msafara huo kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wachezaji hao waliruhusiwa kurejea majumbani kwao.
Mtoa taarifa huyo amesema kuwa, lengo la kupewa ruhusa ni kwenda kusalimia na kukaa kidogo na familia zao baada ya Sikukuu ya Eid al-Fitr kushindwa kusherehekea pamoja wao wakiwa Nigeria.
Ameongeza kuwa wachezaji hao wanatarajiwa kuingia kambini leo Jumatano (April 26) asubuhi kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Rivers United.
“Wachezaji wote waliruhusiwa kurejea majumbani kwao kwa ajili ya kusalimia na kukaa pamoja na familia zao baada ya kurejea kutoka Nigeria.
“Siku hiyo inawatosha wao kukaa pamoja na familia zao kabla ya leo Jumatano asubuhi kuingia kambini na jioni kuanza maandalizi ya mchezo marudiano,” amesema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo Nabi alisema kuwa: “Nimetoa siku moja ya mapumziko kwa wachezaji wangu baada ya uchofu wa safari na mchezo tuliocheza, tulikuwa nje ya nchi kwa zaidi ya siku tano, hivyo nimetoa nafasi kwa wachezaji kwenda kusalimia familia zao.”