Rais wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said amesema, tayari wameshakamilisha maandalizi ya safari ya kuelekea Tunisia, kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans imepangwa Kundi D katika Michuano hiyo, itaanzia ugenini kwa kuikabili US Monastir ya Tunisia Februari 12 mwaka huu.
Injinia Hersi amesema wanatarajia kikosi chao kitaondoka jijini Dar es salaam mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC, utakaopigwa Jumamosi (Februari 04), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
“Maandalizi yote yamekamilika kwa kiasi kikubwa, mchezo wetu unatarajiwa kuwa Februari 12 mwaka huu, hivyo tunajiandaa kuhakikisha kikosi kinasafiri mara tu baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC (Jumamosi hii),” amesema Injinia Hersi Said.
Baada ya mchezo dhidi ya US Monastir, Young Africans itarejea nyumbani Dar es salaam kucheza dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo Februari 19, kisha itakwenda nchini Mali kuikabili Real Bamako, katika Uwanja wa du 26 Mars, mjini Bamako Februari 26.
Machi 08, Young Africans itacheza Mchezo wa Mzunguuko wa Nne wa Kundi D dhidi ya Real Bamako Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Kabla ya kuikaribisha US Monastir Machi 19.
Wananchi watamalizia ugenini kwa kukabili TP Mazembe mjini Lubumbashi katika Uwanja wa TP Mazembe, April 02.