Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yondani awavuruga vigogo Geita

Yondani Geita G Yondani awavuruga vigogo Geita

Sat, 17 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Geita Gold wamekuwa na vikao vya mara kwa mara huku ajenda kubwa ikiwa ni kujadili maboresho ya kikosi chao katika dirisha dogo pamoja na kuanza mikakati ya kuwabakisha wachezaji ambao mikataba yao inaenda ukingoni.

Miongoni mwa mastaa ambao mikataba yao inamalizika ni beki mkongwe, Kelvin Yondani ‘Corton Juice’ ambaye taarifa zinadai ameanza mazungumzo mapya licha ya wachezaji wengi kutaka kuondoka kutokana na ukata wa kifedha unaoikumba timu hiyo.

Akizungumza Katibu Mkuu wa Geita, Liberatus Pastory alisema wanaifanyia kazi ripoti ya kocha wao, Fredy Felix ‘Minziro’ hivyo maamuzi ya mwisho ya nani atabaki au kuondoka yatajulikana baadaye.

“Hatuwezi kusema kwa sasa hivi ni nani ataondoka lakini tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji wetu ambao mikataba inaisha na tukifikia makubaliano tutabaki nao ila tukishindwana tutawafungulia milango,”

“Ni kweli Yondani anamaliza mkataba wake ila tunapambana kumshawishi abaki kutokana na umuhimu wake kwenye kikosi chetu japo changamoto pekee inayojitokeza anataka fedha nyingi ambazo hatuwezi kuzimudu,” alisema.

Wakati Pastory akizungumza hayo taarifa ambazo Mwanaspoti linazo ni kwamba Mwenyekiti wa klabu hiyo, Leonard Bugomola yupo mstari wa mbele kuhakikisha anampa stahiki zake zote beki huyo anazozihitaji ili aendelee kusalia tena.

Awali Kocha Minziro alikaririwai akisema licha ya nyota huyo kumaliza mkataba ila bado anamuhitaji kwenye timu yake kwani uzoefu alionao umewasaidia katika mzunguko wa kwanza.

Licha ya mazungumzo hayo kwa Yondani ila mastaa wengine wanaoweza kuondoka ni mshambuliaji Mkongomani, Erick Yema na beki wa kushoto, Adeyum Saleh ambaye taarifa zinadai tayari amemalizana na Dodoma Jiji dirisha hili.

Chanzo: Mwanaspoti