Yanga inaendelea kujifua Dar es Salaam ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa raundi ya pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE SA ya Ethiopia utakaopigwa Jumamosi ijayo jijini Addis Ababa, huku beki wa kulia wa timu hiyo, Yao Kouassi akikoleza moto baada ya kurejea uwanjani kutoka majeruhi.
Beki huyo aliyekuwa ameumia mazoezini wakati wakijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, ameshusha presha ya watu wa benchi la ufundi akiwamo kocha Miguel Gamondi, baada ya kuanza mazoezi makali na wenzake.
Muivory Coast huyo anayeitumikia Yanga kwa msimu wa pili sasa aliyesajiliwa kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast, amekuwa ni panga pangua katika kikosi cha Gamondi akijizolea umaarufu kwa uwezo wa kulinda lango na kutengeneza mashambulizi yanayoibeba timu katika michuano mbalimbali.
Msimu uliopita Yao alimaliza akiwa na bao moja na asisti saba katika Ligi Kuu Bara akizidiwa na Kipre Junior aliyekuwa Azam aliyeasisti mara tisa na Stephane Aziz KI aliyekuwa na asisti nane, na hivi karibuni aliumia goti la kulia na kulazimika kupumzishwa kwa muda ili kupewa matibabu, lakini kwa sasa yupo fiti.
Kwa sasa staa huyo ameanza mazoezi makali tangu Jumatano, wiki hii, chini ya kocha wa viungo wa timu hiyo, Taibi Lagrouni, ambaye ndiye anayesimamia mpango mzima wa kumuwahisha uwanjani beki huyo.
Ikumbukwe kuwa msimu uliopita wakati Yanga ikitinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliwakosa viungo Pacome Zouzoua, Khalid Aucho na beki huyo kutokana na majeraha, hivyo kurejea kwa Yao mapema kumeleta faraja kwa mashabiki wa klabu hiyo waliombatiza jina la Jeshi.
Yanga itavaana na CBE baada ya kila moja kuvuka raundi ya kwanza ya michuano hiyo, vijana wa Gamondi wakiing’oa kwa kishindo Vital’O ya Burundi kwa ushindi wa mabao 10-0, huku Wahabeshi wakiitoa SC Villa ya Uganda kwa mabao 2-1.