Ni kweli tunahitaji wachezaji 12 wa kigeni kwa timu zetu? Sina hakika. Kila nikitazama orodha ya wachezaji 12 waliojiunga na timu zetu siwaoni. Kuna muda naona wawili. Kuna muda naona wanne.
Pale Simba, nimewaona wawili wa uhakika na mmoja wa kumsubiria. Hakuna wasiwasi wowote kwa Che Malone, huyu beki anaonekana ni mtu na nusu, ni mtu kazi kweli kweli. Anacheza mpira mwingi sana wa kiume. Che Malone ni kama mtoto wa Magomeni Mapipa. Ni kama mtoto wa mjini.
Mzuri sana wa mipira ya juu na mipira ya chini. Ni mara chache sana unapata mtu mwenye sifa hizi. Namheshimu sana Pascal Wawa na nimekuwa nikikiri mbele za watu lakini nadhani Che Malone anakuja kuleta kitu tofauti kwenye ligi yetu.
Akicheza na Henock Inonga hakuna neno. Ukimpanga na Kennedy Juma kote hana neno. Niliposikia Simba wamemsajili MVP wa Cameroon ambaye ni mlinzi wa kati, nikahisi tu atakuwa mtu kazi.
Kuwa mchezaji bora wa ligi wakati unacheza nafasi ya ulinzi, sio jambo la kitoto. Lazima uwe mtu na nusu. Haya ndiyo mambo ya Che Malone.
Sihitaji muda mwingi kumwangalia. Sina wasiwasi wowote. Namwona ni aina ya mchezaji ambaye Simba wamelamba dume. Una wasiwasi na Che Malone? Mimi kiukweli sina shaka naye. Simba wamelamba dume.
Wapo wachezaji ukimwona mara moja tu, unajua ana kitu. Hauhitaji mechi 20 kuthibitisha uwezo wake na nilishangaa sana kuona mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii anaanzia benchi.
Fabrice Ngoma sio mchezaji wa kuanzia benchi mechi yoyote muhimu ya Simba. Ni fundi mitambo kweli kweli.
Ukongwe na uzoefu wake unamfanya kuwa mtulivu sana kwenye kiungo. Wakati timu inashambuliwa, utaona ubora wake kwenye kupora mipira na kuziba nafasi wapinzani wasilete madhara lakini, ni mzuri pia wakati timu ina mpira kwa sababu miguu yake ni kama sumaku.
Akiuita mpira, unaitika, nafurahia sana kumwona kwenye ligi yetu. Nadhani ni mchezaji wa daraja la juu sana ambaye hahitaji mechi nyingi kueleweka.
Ni moja ya usajili mwingine mzuri usiohitaji muda kuzoea mazingira. Nimemwona Onana na Kramo.
Hawa Wachezaji wote wanahitaji muda kidogo kuanza kutengeneza heshima. Ni wachezaji wazuri lakini bado kwa Simba wanahitaji muda wa ziada, Che Malone na Ngoma gari limewaka asubuhi tu.
Umemwona nani anayekuvutia pale Simba? Mimi ni Che Malone na Ngoma hao wengine nahitaji muda zaidi kuwatazama na kujiridhisha.
Umemwona Maxi Nzengeli? Kwa wenye haraka sana pale Yanga tayari wamempa jina la Kylian Mbappe! Bwana mdogo ni fundi kweli kweli. Ni kijana mwenye nguvu na maarifa na kasi ya ajabu.
Haihitaji mechi 20 kuona uwezo wake, kama kuna usajili wa maana sana Yanga wamefanya msimu huu, basi ni huu wa Maxi.
Nimemuona kwenye mechi dhidi ya Kaizer Chiefs kwenye kilele cha Siku ya Mwananchi. Moto wa Nzengeli ulikuwa uleule. Miguu yake ya dhahabu. Mikimbio ya kininja.
Ni kiwanda cha kuzalisha mabao pale Yanga. Ni aina ya mchezaji mwingine ambaye hauhitaji mechi nyingi kumwona kuthibitisha ukubwa wake na kuuamini uwezo wake.
Hawa ndio aina ya wachezaji wanaostahili kuja kwenye ligi yetu. Hakuna ubishi wowote Ligi ya Tanzania ndiyo ligi bora ukanda wetu wa CECAFA. Mpira wetu unaingiza pesa nyingi sana na ndiyo maana kina Nzengeli wanakuja. Tuko matawi ya juu sana.
Nimemwona Nzengeli mechi ya Azam FC na Simba pale Mkwakwani. Mwendo ni uleule na ufundi ni uleule. Ni kijana aliyekamilika kila kitu, nasubiri ligi ianze tuanze kuhesabu mabao na pasi za mabao na kuona watu wanakimbizwa na Nzengeli. Kama atakuwa fiti msimu mzima, namuona akiwa msaada mkubwa sana kwa Yanga.
Kuna mwanaume mwingine pale Jangwani anaitwa Yao Yao. Ni Jina lake Jipya. Anajulikana kama Kouassi Attohoula Yao. Ni Beki katili wa kulia. Huyu jamaa anajua sana. Moja kati ya usajili mwingine ambao Yanga wamepatia. Ni Beki katili mwingine aliyeongezeka kwenye ligi yetu.
Nawaona Yanga wakiwa na ukuta wa chuma msimu huu, Yao ni miongoni mwa usajili ambao binafsi sina shaka nao. Ni mchezaji mwenye nguvu na mapafu ya mbwa.
Bila shaka yoyote alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kumdhibiti Clatous Chota Chama kwenye mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii. Hakuna asiyejua ufundi wa Chama.
Yao anaonekana kumudu aina zote za uchezaji. Ukiketa uhuni yumo, ustaarabu pia yumo. Namwona ni mchezaji anayeweza kumudu ligi yetu kwa haraka.
Nimewaona wachezaji wengine pia lakini nadhani wanahitaji muda. Hawa wawili kutoka Jangwani, nadhani wako tayari kwa ligi yetu. Hawahitaji chochote kuzoea ligi. Kama umwona mchezaji mwingine wa kigeni kutoka pacha wa Kariakoo uliyemkubali, tafadhali usisite kunijuza kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.