Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yazindua kitabu cha historia

GQJB2sVWgAA75kq.jpeg Yanga yazindua kitabu cha historia

Sun, 16 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga SC, jana usiku ilizindua kitabu kinachoonyesha historia nzima ya klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake kilichopewa jina la Klabu Yetu, Historia Yetu.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo sambamba na viongozi wa Serikali huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko.

Akizungumza katika uzinduzi wa kitabu hicho chenye kurasa 251, Rais wa Yanga SC, Injinia Hersi Said, amesema;

“Namshukuru Mzee Mudhihir Mudhihir ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uandaaji wa kitabu hiki cha historia ya Yanga akishirikiana na Mzee Mhende na wengineo. Yanga imewaamini na kuwakabidhi jukumu hili na historia itaendelea kuwakumbuka.

“Kitabu hiki kitakuwa na kurasa 251, vilevile kitabu hiki kitakuwa kwenye mitandao yetu ikiwepo App ya Yanga ambapo unaweza kukisoma kupitia simu yako au kompyuta yako,” aliongeza Injinia Hersi.

Mgeni rasmi, Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko, alisema: “Mheshimiwa Rais ametuma nije nimuwakilishe kwenye uzinduzi wa kitabu. Mheshimiwa Rais amewatakia Yanga kila la kheri kwenye uzinduzi wa kitabu hiki. Makamu wa Rais na Waziri Mkuu nao wametuma salamu.

“Nimpongeze Rais wa Yanga kwa kuwaamini waandishi wetu wazalendo kuandaa kitabu hiki. Nimefurahi sana kuona kamati hii ikiwa na waandishi wakongwe. Mimi binafsi napenda sana kusoma, kuanzia sasa nami nitatenga muda wangu kwa ajili ya kusoma kitabu hiki.”

Yanga imezindua kitabu hicho ikiwa ni mwaka mmoja umepita baada ya kuzindua Documentary iliyoonyesha mafanikio ya Yanga iliyoyapata msimu wa 2022-2023 ikiwemo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935 ndio inayoshikilia rekodi ya kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu Bara ikifanya hivyo mara 30, ikifuatiwa kwa mbali na Simba yenye 22 huku Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja ikiwa ya tatu na mataji mawili, ilihali Cosmopolitan, Mseto, Pan Africans, Tukuyu Stars, Coastal Union na Azam FC zikifunga hesabu kwa kila moja kutwaa mara moja moja.

Pia ilikuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua ya robo fainali mara mbili mfululizo 1969 na 1970 kisha kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza nchini kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998 mara Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilipobadilisha michuano hiyo kutoka Klabu Bingwa Afrika 1997.

Kadhalika ilikuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili tangu CAF ilipoianzisha michuano hiyo kwa kuunganisha Kombe la Washindi na Kombe la CAF mwaka 2004 na mwaka jana ikafika fainali ikiboresha zaidi rekodi hiyo barani Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: