Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yazima Propaganda za kuwanyima Ubingwa

Kikosi Yanga 15 Nyota wa Yanga, waambiwa wasisikilize chochote kwa sasa

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga inaendelea kupiga hesabu zao za ubingwa msimu huu, lakini ghafla wakashtukia jambo baada ya kuenea tetesi straika wao mkali wa kufumania nyavu, Fiston Mayele anatakiwa klabu ya Kaizer Chiefs na fasta wakamwambia jamaa ye aendelee kucheka na nyavu tu ili wasiyumbe.

Katikati ya wiki kulizuka taarifa Mayele mwenye mabao 10 na asisti tatu anatakiwa na klabu hiyo ya Afrika Kusini na mmoja wa vigogo wa Jangwani, aliamua kuingia chimbo kusaka taarifa hiyo na kubaini ni kanyaboya yenye lengo la kuitaka kuwavuruga katika mbio zao za kuwania ubingwa na hapo hapo akaamua kumwita straika huyo na kuzungumza naye asivurugwe na taarifa hizo na badala yake azidi kufunga zaidi.

Akizungumza Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa alisema ameshtukia taarifa za ofa ya Mayele kutakiwa na Kaizer Chiefs ni propaganda za kutaka kumpunguza kasi mshambuliaji wao huyo aliye katika kiwango bora.

Senzo ambaye ni raia wa Afrika Kusini, alisema mapema alifuatilia taarifa hizo hadi Afrika Kusini na ndani ya Kaizer na kugundua ni uzushi tu na haraka wakamweka chini Mayele na kuzungumza naye.

Alisema kama viongozi wamemwambia Mayele anatakiwa kuendelea kufunga na kama kungekuwa na ofa yoyote ya kutoka Kaizer, basi Bobby Motaung ambaye ni bosi wa mambo ya ufundi wa klabu hiyo angekuwa wa kwanza kuwasiliana naye.

“Hizi ni propaganda tu, sikwambii hivi kwa maana ya kukanusha tu, ila nimefuatilia hadi Kaizer ndani, hakuna huo ukweli, unajua wapo wengine wanazisikia klabu kama Kaizer, Orlando Pirates au Mamelodi Sundowns lakini kwangu ni tofauti,” alisema na kuongeza;

“Kama Kaizer watamtaka Mayele au kutaka chochote kutoka Yanga nafikiri kama sio mimi basi ndugu yangu Hersi (Said) atakuwa wa kwanza kujua tuna Boby pale (Motaung) angetujulisha haraka.”

Senzo aliyewahi kufanya kazi Orlando Pirates kabla ya kuja nchini kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba na baadaye kutua Yanga, alisema; “Haya ni mambo yanayotokea kwa lengo la kumfanya mchezaji asijitume apunguze kasi yake kuanza kufikiria ofa ya kutaka kuondoka, tupo kwa muda mrefu hapa Tanzania tunajua hili, tumemwambia Mayele taarifa hizi zimfanye aongeze kasi na timu zinazokuja azifunge.”

Naye Meneja wa mchezaji huyo, Nestor Mutuale alipotafutwa na Mwanaspoti alisema “Sijapokea ofa ya namna hiyo, tunaona tu taarifa katika mitandao, nafikiri kuna mtu atakuwa ameamka na kuamua kuandika kitu bila uhakika, Kaizer ni klabu kubwa inajua jinsi ya kufanya mawasiliano, ikizingatiwa Mayele ana mkataba Yanga, ebu tuwaachie Yanga wao ndio wanaommiliki mchezaji,” alisema Mutuale raia wa DR Congo.

Mayele amekuwa katika kiwango bora na katika mechi 17 za Ligi amefanikiwa kufunga mabao 10 na kutoa pasi tatu za mabao akiwa ndio kinara wa ufungaji sambamba na mshambuliaji wa Namungo Reliant Lusajo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live