Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yawakosa mastaa watano

Guede X Metacha Yanga yawakosa mastaa watano

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Ligi Kuu Bara ikirejea baada ya kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, Yanga inaanza na mechi ya kiporo dhidi Kagera Sugar katika mchezo unaopigwa leo kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mechi hiyo inayoanza saa 10:00 jioni, inatarajiwa kuwa na ushindani na burudani ya aina yake kutokana na timu hizo kupata muda mrefu wa kujiandaa na pia kuongeza nguvu vikosini kwa kufanya usajili katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu.

Timu zote mbili zitaingia kwenye mechi hiyo zikiwa zimetoka kucheza mechi za Kombe la Shirikisho (ASFC), Jumanne ya wiki hii ambapo Yanga ilikipiga dhidi ya Hausung FC kutoka Njombe na kushinda mabao 5-1, huku Kagera ikiichapa Dar City ya Dar es Salaam mabao 4-0.

Katika mechi hiyo Yanga itawakosa wachezaji watano ambao ni mabeki Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca' pamoja na winga mpya Augustine Okrah amao ni majeraha, kipa Djigui Diarra aliyepo kwenye fainali za Afcon na kiungo Stephane Aziz Ki ambaye hajarejea kutoka kwenye timu ya taifa 'Burkina Faso'.

Hata hivyo, wachezaji wengine wapya mshambuliaji Joseph Guede na kiungo Shekhan Hamis wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi.

Kwa upande wa wenyeji, Kagera Sugar itaingia uwanjani ikiwa na mabadiliko kwenye benchi la ufundi ambapo kocha mkuu Fred Felix 'Minziro' alitambulishwa juzi kuchukua mikoba ya Mecky Maxime aliyeachwa na baadaye kutimkia Ihefu SC. Pia itakuwa na sura mpya uwanjani za viungo Geofrey Manyasi na Mubaraq Amza.

Kagera Sugar itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya dhidi ya Yanga kwani katika mechi tano za ligi zilizopita kati ya timu hizo, imefungwa nne na kutoka sare moja.

Pia matokeo ya mechi tano za Yanga zilizopita katika ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika zinaibeba zaidi kwani imeshinda tatu na sare mbili, huku Kagera Sugar ikishinda moja, sare moja na kupoteza tatu katika mechi tano za ligi.

Hadi sasa Kagera Sugar imecheza mechi 13 za ligi ikishinda tatu, sare nne na kupoteza sita ikivuna alama 13 na kukalia nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa imefunga mabao manane na kufungwa 16, huku Yanga ikiwa nafasi ya pili na alama 30 baada ya mechi 11, ikishinda 10 na kupoteza moja, ikifunga mabao 31 na kuruhusu sita.

Kama Yanga itashinda leo itapaa hadi kileleni mwa msimamo kwani itafikisha pointi 33 na kuishusha Azam FC yenye 31. Sare au kupoteza mechi itaifanya kusalia katika nafasi ya pili.

Kwa upande wa Kagera, ushindi utaifanya kufikisha alama 16 na kusogea hadi nafasi kati ya 10 au 12, ikitegemea na mabao itakayofunga na kufungwa, ilhali sare itaisogeza hadi nafasi ya 13 na kupoteza mchezo kutaifanya kusalia ya 14.

Wakizungumzia mchezo huo, kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi na msaidizi wa Kagera Sugar, Marwa Chamberi walitambiana kwamba wamejipanga vyema na kila mmoja akitaka alama tatu zinazowaniwa na pande hizo.

"Lengo ni ushindi. Tunatarajia kuwa na mechi nzuri na wachezaji wapo tayari kupambana kuhakikisha wanaipa timu alama tatu," alisema Gamondi.

Naye Marwa alisema: "Tumejipanga kushinda. Tunatambua Yanga ni timu kubwa, ina wachezaji wengi wenye ubora wa juu. Tutacheza kwa kuwaheshimu huku lengo kuu likiwa ni kutafuta ushindi."

Chanzo: Mwanaspoti