YANGA imeichapa JKT Tanzania bao 1-0 katika mechi ya kirafiki, iliyopigwa Uwanja Avic Town, uliopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Bao la Yanga lilifungwa na Athuman Yusuf liliyoanzia kwa Saido Ntibanzonkiza aliuchopu mpira ukamkuta Makambo aliyetoa asisti ya bao hilo kipindi cha kwanza.
Ilikuwa mechi ya kipimo sahihi kwa Yanga ambao walitumia wachezaji ambao hawakucheza mechi ya KMC Songea na wale waliocheza dakika chache kutokana na ushindani ambao waliuonyesha JKT Tanzania, ambao Jumamosi wanakutana na Ndanda FC mechi ya Championship huku Yanga ikiivaa Azam FC kwenye NBC Ligi Kuu.
Kipindi cha pili JKT Tanzania ilipambana ili kusawazisha bao, kazi nzuri ya mabeki Abdallah Shaibu 'Ninja', Adeyum Saleh wakisaidiana na kiungo mkabaji Mukoko Tonombe ambao waliweka ulinzi mzuri.
Makocha wa timu hizo, walionekana kuwa makini kuutazama mchezo huo, wakiutumia zaidi kuwaelekeza namba ya kusimama katika nafasi zao.
Kocha Nabi alionekana zaidi kuzungumza na Saido ili kumsaidia kuwaelekeza wachezaji wengine kuzingatia maelekezo yake. Mwisho.