Ushindi wa mabao 5-1 ilioupata Yanga dhidi ya Simba leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, imevunja rekodi ya kutopoteza mchezo wa Ligi Kuu Bara kwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mbrazili, Roberto Oliveira maarufu 'Robertinho'.
Robertinho aliyejiunga na Simba Januari 3, mwaka huu, alikuwa hajapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu uliopita kwani kabla ya mchezo wa leo wa 'Derby ya Kariakoo' aliiongoza timu hiyo kushinda jumla ya mechi 15 huku miwili pekee ikiisha kwa sare.
Mbali na hiyo ya Robertinho ila pia Yanga imevunja rekodi ya Simba ya kutopoteza mchezo wa Ligi Kuu Bara kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Azam FC bao 1-0, la Prince Dube Oktoba 27, mwaka jana ilikuwa imecheza jumla ya michezo 29 ambapo kati yake ilikuwa imeshinda 24 huku mitano ikiisha kwa sare.
Huu ni mchezo wa 111 kwa timu hizi kukutana katika Ligi Kuu Bara ambapo Yanga imeshinda 39, sare 40 huku Simba ikishinda 32 wakati Yanga imefunga mabao 118 na kuruhusu 104.
Tangu 1965 Simba Na Yanga zimekutana katika michezo 37 iliyochezwa siku ya Jumapili Ambapo Simba Imeshinda 10, vichapo vinane na sare 19.
Yanga Ilikuwa ni timu ya kwanza kushinda mchezo wa Jumapili baada ya kuifunga Simba bao 1-0, Juni 18, 1972 lililofungwa na Leonard Chitete.
Mchezo wa kwanza kupigwa Jumapili ulikuwa ni wa Juni 4, 1972 zikifungana bao 1-1 huku Simba (Sunderland) ikipata bao kupitia kwa Willy Mwaijibe wakati la Yanga lilichomolewa na Kitwana Manara.
Mechi ya mwisho iliyopigwa Jumapili baina ya timu hizi katika Ligi Kuu Bara Simba ilishinda mabao 2-0, Aprili 16 mwaka huu yaliyofungwa na nyota wa timu hiyo, Henock Inonga na Kibu Denis.