Mpango wa Rivers United ya Nigeria kutaka kuwapeleka mabingwa wa Tanzania, Yanga kwenye Uwanja wa Adokiye Amiesimaka, Port Harcourt umegonga mwamba na badala yake mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utapigwa Godswill Akpabio, Uyo.
Rivers walikuwa wakitarajia kupata kibali kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kurejea katika uwanja wao wa nyumbani, wa Adokiye Amiesimaka, Port Harcourt baada ya ukarabati mkubwa kukamilika.
Lakini maombi hayo yametupiliwa mbali na Caf na badala yake wataendelea kucheza michezo yao ya nyumbani kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio.
Rivers wako nafasi ya pili kwenye kundi lao katika Ligi Kuu ya Soka ya Nigeria (NPFL), watalazimika kuendeleza kampeni yao ya kimataifa uwanjani hapo ambapo walicheza michezo yote ya hatua ya makundi.
Baada ya ukaguzi wa awali uliofanyika kwenye Uwanja wa Adokiye Amiesimaka, inatarajiwa kuwa CAF itatuma kikosi kingine ili kuthibitisha matokeo hayo lakini inaonekana hakutakuwa na muda wa kutosha kufanya hivyo kabla ya mchezo wa robo fainali dhidi ya Yanga.
Ikicheza Uyo, Rivers United ilivuna pointi saba kati ya tisa na kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi B na kutinga hatua ya mtoano ya michuano hiyo ambapo sasa itamenyana na Yanga Jumapili.
Rivers wana hofu ya kutumia uwanja huo kutokana na kutokuwa na mashabiki wao wengi. Mwamuzi wa Afrika Kusini Abongile Tom ameteuliwa na CAF kuchezesha mchezo huo.
Hii si mara ya kwanza kwa timu zote mbili kuchuana katika michuano ya CAF. Septemba 2021, Rivers United iliifunga Yanga nyumbani na ugenini katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.