Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yatupwa nje Ligi ya Mabingwa Afrika

Yanga Out CAF Yanga imeishia hatua ya Robo Fainali baada ya kutolewa kwa mikwaju ya penati 3-2

Fri, 5 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imecheza mpira mkubwa lakini imeshindwa kuamua mechi na kujikuta ikiondolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mikwaju ya penalti 3-2 mbele ya Mamelodi Sundowns nchini Afrika Kusini.

Timu ya Wananchi ilikwenda Afrika Kusini ikiwa inahitaji kupata japo sare ya mabao baada ya mechi yao ya awali jijini Dar es Salaam kumalizika kwa suluhu, lakini ikashindwa kupata ushindi licha ya kutengeneza nafasi nzuri zaidi katika mechi zote mbili – zikiwamo za wazi zaidi za Clement Mzize nchini Afrika Kusini na hata Dar es Salaam.

TATIZO NI HILI

Yanga ilipungua ukali kutokana na kuwakosa katika mechi zote mbili nyota wao watatu muhimu wa kikosi cha kwanza ambao ni uti wa mgongo wa timu hiyo, beki wa kulia Yao Kouassi, kiungo wa ulinzi Khalid Aucho na kiungo wa ushambuliaji, Pacome Zouzua kutokana majeraha.

Lakini licha ya kuwakosa wakali hao, Yanga bado ilicheza vyema kwa nidhamu ya hali ya juu katika mechi zote mbili dhidi ya mabingwa hao wa Afrika wa kombe jipya la AFL ndani ya dakika zote 180, ni Yanga iliyokaribia zaidi kufunga kwa shuti lile la Aziz Ki na pia ikipoteza nafasi nyingi za wazi.

Mechi hizi mbili pia zimethibitisha wazi ni kwanini Yanga inahitaji kumpata mshambuliaji wa kiwango cha juu baada ya kuondoka kwa Fiston Mayele.

BASI LA YANGA

Kama kuna kitu ambacho kocha Miguel Gamondi alifanikiwa basi ni mfumo wa kujilinda aliorudi nao kwenye mechi hiyo ambao uliwaweka kwenye wakati mgumu Mamelodi kushindwa kuwa na mchezo rahisi mjini Pretoria kama ilivyokuwa nyumbani Dar es Salaam.

Gamondi ambaye alianza na mfumo wa 4-4-2, vijana wake wanne wa kati walifanya kazi kubwa kufunga njia za wenyeji kukamilisha mashambulizi yao kupitia katikati na kuwafanya Mamelodi kutumia upande wa pembeni kumwaga mashambulizi lakini bado Yanga ilikuwa imara.

Wakati Mamelodi ikiwa kwenye nusu ya Yanga wageni walikuwa wanajikuta wako 9-10 dhidi ya wenyeji 7-8 na kuweka ugumu kwa Masandawana kukamilisha mashambulizi yao.

BACCA, DIARRA KAZI KUBWA

Wakati Mamelodi ikitumia njia za pembeni kupandisha mashambulizi bado ikakutana na uzito kutoka kwa ulinzi wa Yanga wakiongozwa na beki Ibrahim Hamad 'Bacca' ambaye alikuwa imara kucheza mipira ya kichwa wakati kipa wake Djigui Diarra akionyesha ubora wa kucheza krosi za wenyeji na kupoza presha ya mechi.

BAHATI YA LOMALISA

Ndani ya dakika 16 za kwanza Yanga ilinusurika kucheza pungufu baada ya beki wake Lomalisa Mutambala kumchezea vibaya beki Khuliso Mudau kisha kupewa kadi ya njano na mwamuzi Dahane Beida kutoka Mauritania.

Baada ya kadi hiyo bado mwamuzi Beida akarudishwa kulitazama tukio hilo kwa mara ya pili kwenye VAR lakini bado Beida akasimamia uamuzi wake na Lomalisa kunusurika kadi nyekundu.

MKUDE DAH!

Kiungo Jonas Mkude ambaye alisifiwa kwa kucheza vyema mechi ya Dar es Salaam, alikuwa imara tena akivuruga mipango ya Masandawana, lakini kati ya makosa adimu aliyofanya katika mechi hiyo nusura liigharimu mapema Yanga katika dakika ya 38 pale alipompasia kimakosa winga wa Mamelodi, Thembinkosi Lorch ambaye angekuwa makini angeifunga Yanga lakini akapoteza nafasi hiyo pale shuti lake lilipotoka nje kidogo.

YANGA BILA SHUTI 45 ZA KWANZA

Mpaka dakika 45 za kwanza zilipomalizika Yanga ilipiga mashuti mawili wakati Mamelodi ikipiga mashuti manne lakini ni shuti moja tu lililolenga lango lililopigwa na wenyeji huku wageni wakiwa hawana shuti lililolenga lango.

UTATA SHUTI LA AZIZ KI

Yanga ililalamikia kunyimwa bao katika dakika 59 pale Stephanie Aziz KI alipopiga shuti na mpira kugonga besela kabla ya kudunda chini ukiaminika umeingia wavuni, lakini VAR ikaamua sio bao na kuzua utata wa uhalali wa uamuzi huo kufanyika bila ya kuwepo kwa teknolojia ya ‘goal line’.

Aziz Ki, ambaye amekuwa akihusishwa na mipango ya kutimkia Mamelodi mwisho wa msimu huu wakati mkataba wake utakapomalizika huku akiwa hajasaini kuuongeza wa kubaki Yanga, alipiga shuti hilo lililozua utata baada ya kupigiana ‘one-two’ na Kennedy Musonda.

Shuti hilo lilimfanya Azizi kuanza kuishangilia huku Mamelodi wakidai sio bao kisha VAR ikamsaidia tena refa Beida kuamua kuwa halikuwa bao.

Yanga pia ilipoteza nafasi nyingine dakika ya 78 kupitia mshambuliaji wake Clement Mzize aliyeingia katika dakika ya 68 akichukua nafasi ya Musonda aliyepata maumivu pale alipopokea pasi safi kutoka kwa Aziz Ki lakini akapiga nje akiwa hatua chache langoni.

Mpaka dakika 90 zinakamilika timu hizo zilimaliza kwa suluhu nyingine na kuifanya mechi hiyo kwenda kuamuliwa kwa ‘matuta’ wenyeji wakishinda kwa penalti 3-2.

Kipa wa Mamelodi, Ronwen Williams, ambaye aliokoa penalti nne katika mechi moja ya Afcon 2023 wakati akiitumikia timu yake ya taifa ya Afrika Kusini, ameibuka shujaa kwa Mamelodi baada ya kuokoa penalti mbili za kwanza za Yanga zilizopigwa na Aziz KI, beki Dickson Job huku Bacca akipaisha wakati Augustine Okrah na Guede walifunga.

Mamelodi penalti zao zilifungwa na Marcelo Allende, Lucas Ribeiro na Neo Maema wakati ile ya Leandro Sirino ilipanguliwa na Diarra.

Kipigo hicho kimezima ndoto ya Yanga kwenda nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake na pia kwa mara ya kwanza tangu irejee baada ya kushindwa kufuzu hatua ya makundi kwa miaka 25.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: