Baada ya kuwa kwenye hafla maalumu iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kikosi cha Yanga leo kitakuwa na kazi Mbeya. Wachezaji wa Yanga pamoja na Benchi la ufundi Juni 5, 2023 walikuwa kwenye halfa ya pongezi kwa Yanga kwa kufanikiwa kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Safari kuelekea Mbeya kuikabili Mbeya City ilianza saa 5 usiku ambapo walitumia ndege maalumu iliyotolewa na Serikali.
Leo Yanga ambao ni mabingwa watakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu dhidi ya Mbeya City, Uwanja wa Sokoine ikiwa ni mchezo wa ligi, mzunguko wa pili.
Yanga imetwaa ubingwa ikiwa na mechi mbili mkononi ambazo zimebaki na wanatarajia kuwa na paredi la ubingwa Juni 10, Dar.