Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yatingishwa sakata la GSM

100531 Yanga+pic Yanga yatingishwa sakata la GSM

Sat, 28 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati vigogo watatu wameng’oka madarakani Yanga huku wengine wawili wakisimamishwa, sakata la kampuni ya GMS na klabu ya Yanga limewatofautisha wadau wa soka nchini, huku baadhi wakiipa mbinu klabu hiyo kongwe ya soka kujiendesha kisasa.

Jana wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Said Kambi, Rodgers Gumbo na Shija Richard walijiuzulu, huku wajumbe wengine wawili Frank Kamugisha na Salim Rupia wakisimishwa na Kamati ya Utendaji ikiwa ni presha iliyotokana na mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Kampuni ya GSM kujiondoa katika kutekeleza baadhi ya majukumu iliyokuwa ikiyafanya.

Uamuzi wote huo ulifikiwa baada ya kikao cha siku mbili mfululizo cha Kamati ya Utendaji ya Yanga kilichojadili kujitoa kwa GSM kujitoa udhamini wa masuala yasiyo ya kimkataba.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Mshindo Msolla, ilieleza Kamugisha na Rupia wamesimamishwa kuanzia jana hadi hapo Mkutano Mkuu utakapofanya uamuzi kwa mujibu wa Katiba ya Yanga.

Yanga pia, imewasilisha barua kwa GSM kujibu barua yao Machi 24 kuhusu kujitoa udhamini wa masuala yasiyo ya kimkataba, barua ambayo imewasilishwa ikibeba uamuzi wa pamoja wa Kamati ya Utendaji.

Hivi karibuni, GSM aliandika barua ya kujitoa katika kufanya masuala yaliyo nje ya mkataba kama kulipa bonasi za wachezaji, kusajili wachezaji na kulipa mishahara ya wachezaji na kubakisha yaliyo katika mkataba wa udhamini tu ambayo ni mgawo wa mauzo ya jezi za klabu hiyo.

Pia Soma

Advertisement
Sakati hilo limewaibua baadhi ya wadau wa soka akiwamo aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako na Mkurugenzi wa zamani wa Mashindano wa TFF, Sadi Kawemba.

Kawemba alisema tatizo la Simba na Yanga, viongozi hawaelewi watu walio nyuma ya klabu hizo ni mtaji.

“Wanachokosea ni kusubiri mwenye pesa atoe pesa zake kwa klabu halafu wao wampangie majukumu ya kutumia fedha zake.

“Wenye pesa ndiyo wanaouona huo mtaji Simba na Yanga, mfano GSM akiwauzia wapenzi milioni tatu jezi za Yanga kwa Sh 10,000 kila moja, ataingiza kiasi gani (Sh. 30 bilioni), akitoa bilioni tano kuipa Yanga hatokuwa na hasara.”

Alisema viongozi wa klabu hizo kongwe wanasajili makocha na wachezaji profesheno, lakini wao bado wanaziongoza klabu kwa staili ya soka la ridhaa.

“CEO wa Simba sifa yake kubwa ni kwamba alikaa darasani akafundishwa namna ya kuongoza, lakini viongozi wengi wa klabu zetu kongwe ni aidha kacheza mpira, amewahi kuwa kocha au ni mwanachama mzoefu.

“Pia viongozi hawajui ‘product’ zao, utakuta wanamtegemea mtu mmoja, huyo huyo ndiye anawapa pesa za safari ya ndege, mishahara ya wachezaji, analipa hoteli, sasa akisema anajitoa kusaidia lazima wampigie magoti, wakati kumbe wale wapenzi na wanachama walio nyuma ya timu hizo ni mtaji tosha,” alisema Kawemba.

Beki na Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Mwalusako alisema tatizo la klabu hiyo linaanzia kwa wanachama baadhi ambao wanaitumia klabu kwa maslahi binafsi.

“Yanga ikiamua inaweza kujiendesha kwa michango ya wanachama, mauzo ya jezi na vitu vingine vingi, lakini wapo baadhi ni tatizo na mara nyingi anayeanzisha mpango wa klabu kujiendesha anapigwa vita kweli kweli,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba mwenye pesa ana nguvu, lakini isiwe sababu za mtu kuitingisha klabu na klabu kwenda ‘kumpigia magoti’.

Mtendaji huyo wa zamani wa Yanga alisema Yanga imekuwa ikijitengenezea kuwa klabu maskini, jambo ambalo kama ikiweka mifumo mizuri ya kujiendesha itakuwa moja ya klabu zenye pesa Afrika, japo hilo linahitaji mtu mwenye msimamo kulianzisha kwa kuwa atapigwa vita vikali na kuonekana hafai.

Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Ally Mayay alisema Yanga iko katika kipindi cha mpito kuelekea katika mabadiliko, lakini ni kipindi ambacho wanachama hawataki kuona timu yao inapoteza dira kwenye ushindani. “Katika kipindi cha mabadiliko lazima sapoti ya wadau iendelee, ndiyo sababu Yanga hawataki kumpoteza GSM na wadhamini wake wengine, vinginevyo timu ikubali kupotea kwa miaka mitano ili ikae sawa.”

Alisema kinachotakiwa ni Yanga na GSM ‘kubebana’ mmoja kati yao asijione mkubwa kuliko mwenzake, na si huyo tu, utaratibu huo uwe kwa yoyote aliyeweka fedha zake kuisadia klabu apewe heshima stahiki na klabu vivyo hivyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz