Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yatawala tuzo Ligi Kuu, yatoa onyo

Yanga AAI4lM.jpeg Yanga yatawala tuzo Ligi Kuu, yatoa onyo

Fri, 2 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Stephane Aziz Ki akipokea tuzo ya kiungo bora wa msimu katika tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilizofanyika katika Ukumbi wa Super Dome jijini Dar es Salaam. Picha na Yanga

Dar es Salaam. Yanga imetawala tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana, huku ikiahidi kuchukua zote msimu ujao.

Tuzo hizo kwa ajili ya wachezaji na makocha waliofanya vizuri msimu uliopita zilitolewa kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, huku Aziz Ki akizoa tatu.

Aziz Ki alionekana kutakata kwenye tuzo hiyo baada ya kuchukua tuzo kiungo bora, mfungaji bora, pamoja na mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara 2023/2024.

Kiungo huyo raia wa Ivory Coast, alionekana kustahili kutwaa tuzo hizo baada ya msimu uliopita kucheza michezo 27 ya Ligi Kuu, alifunga mabao 21 yakiwa ni zaidi ya wachezaji wengine wote kwenye ligi.

Alitoa asisti nane na kufunga hat trick mbili kwa msimu mzima ambao Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa. Mbali na kutwaa tuzo hizo, pia Aziz Ki aliibuka kwenye kikosi bora cha msimu akiwa kwenye eneo la kiungo.

Wengine wa Yanga waliotwaa tuzo hizo ni Ibrahim Bacca ambaye alitwaa ile ya beki bora, Miguel Gamondi ambaye alichukua tuzo ya kocha bora wa msimu. Kikosi bora kimeingiza wachezaji sita wa Yanga, ambao ni Yao Kouassi, Bacca, Dickson Job, Mudathir Yahaya, Maxi Nzegeli pamoja na Aziz Ki.

Wachezaji wengine walioingia kwenye kikosi hicho ni Kipa wa Coastal Union Lay Matampi ambaye amechukua tuzo ya kipa bora wa msimu wa Ligi Kuu, Kipre Junior wa Azam ambaye ametwaa tuzo ya bao bora la msimu.

Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho la CRDB.

Beki wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala' akiwa ndiye mchezaji pekee wa timu hiyo aliyekuwa kwenye kipengele cha kuwania tuzo hizo pamoja na mshambuliaji wa KMC, Wazir Junior.

Wengine waliotwaa tuzo ni Mbwana Samatta ambaye alichukua ile ya mchezaji bora kwa Wanaume anayecheza nje ya nchi, Aisha Masaka Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza nje ya nchi, Caroline Rufo alitwaa tuzo ya kipa Bora Ligi ya Wanawake, Leodgar Tenga tuzo ya Heshima ya TFF, Mohammed Mkono tuzo ya Mwamuzi Bora msaidizi, Djigui Diarra alitwaa tuzo ya kipa Bora Kombe la CRDB, Ahmed Arajiga alitwaa tuzo ya Mwamuzi Bora Ligi Kuu.

Wengine ni Juma Mgunda akitwaa tuzo ya kocha Bora Ligi Kuu ya Wanawake, Mtibwa Sugar ilitwaa tuzo ya timu yenye nidhamu huku Clement Mzize akitwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa Kombe la CRDB.

Akizungumza baada ya tuzo hizo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema pamoja na kwamba msimu huu wamechukua tuzo nyingi, lakini kwa kikosi walichonacho msimu ujao watazitwaa zote.

"Msimu huu tumechukua tuzo nyingi, lakini hawa wachache walioingia kwenye kikosi  Bora msimu ujao, hawatakuwepo kwa kuwa tuna timu bora zaidi. Nimemuona Mohammed Hussein kwenye eneo la beki kwenye kikosi, huyu ni mmoja kati ya wachezaji ambao nawaheshimu sana kwenye soka hapa nchini, tena sana, lakini msimu ujao hatakuwepo, tutatawala kikosi kizima cha msimu," alisema Kamwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: