Klabu ya Soka ya Yanga kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Kamati ya Uchaguzi Malangwe Ally Mchungahela imetangaza tarehe rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa Klabu hiyo ambayo ni Julai 10, 2022.
Mchungahela amesema Uchaguzi Mkuu utahusisha nafasi za Rais wa Timu, Makamu wa Rais na Wajumbe Watano (5).
Na mchakato wa uchaguzi huo unaanza mara moja ambapo Juni 5-9, 2022 zoezi la kuchukua fomu linafunguliwa rasmi likifuatiwa na zoezi la mchujo wa wagombea litakalofanywa kuanzia Juni 10-11, 2022 likitekelezwa na Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Yanga.
Michakato mingine itaendelea huku ratiba kamili ya michakato hiyo hadi kufikia tarehe rasmi ya zoezi la Uchaguzi Mkuu inatarajiwa kubandikwa katika mbao za matangazo Makao Makuu ya Klabu hiyo.
Lakini Pia Mchungahela ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ameongeza muda wa wki mbili kwa matawi yte ya Klabu ya Yanga nchini Kukamilisha zoezi la uchaguzi wa viongozi kwa ngazi zao kisha nyaraka za Muhtasari na maazimio ya chaguzi hizo ikiwemo Viongozi waliochaguliwa ziwasilishwe Ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu hiyo Senzo Mbatha Mazingiza.
Mwenyekiti huyo amekumbusha matawi yote kuwa viongozi wanaotakiwa kuchaguliwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Mweka Hazina na Wajumbe Watano lakini pia wachaguliwe Wajumbe wengine Wawili ambao watawakilisha Matawi katika Uchaguzi Mkuu wa Julai 10, 2022.