Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yataka rekodi mbele ya Geita Gold

Yanga FC Kambi Yanga yataka rekodi mbele ya Geita Gold

Sat, 29 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

​​​​​​​Wakati Yanga ikipania kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi ya 45 mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara leo itakapovaana na Geita Gold kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wenyeji wa mchezo huo wameapa kumaliza mfululizo wa timu hiyo kucheza mechi bila kupoteza.

Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe amesema baada ya mechi dhidi ya KMC, wanarejea wakiwa na baadhi ya wachezaji ambao hawakuwepo kwenye mechi iliyopita.

"Tunajua ugumu wa mechi, haitokuwa rahisi kwa sababu Geita Gold ni timu ngumu, lakini sisi tuna wachezaji wazuri na maandalizi bora zaidi. Kuna waliosema kuwa tunataka kuendeleza rekodi yetu ya kucheza mechi mfululizo bila kupoteza, ni kweli hatujapoteza, lakini hatujiandai kwa ajili ya kulinda rekodi, ila tumefanya maandalizi ya mchezo husika," alisema Kamwe.

Wachezaji ambao walikosekana kwenye mechi dhidi ya KMC Jumatano iliyopita ni Fiston Mayele, Khalid Aucho, Kibwana Shomari ambao walipumzishwa, na Bernard Morrison ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha mechi tatu.

"Kwenye mechi hii hatujaja na Mwamnyeto kwa sababu ya plan tu ya mwalimu, tuna mechi nyingi mfululizo hivyo kwa plani yake na ushahuri wa wataalam wa afya, wameshauri tuwe makini kuhakikisha tunalinda afya zao kwa kuwapumzisha ili tupate ufanisi wao kwa asilimia mia moja," alisema Kamwe.

Kwa upande wa Geita Gold, Kaimu Katibu Mkuu Liberatus Pastory alisema maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika chini ya Kocha Mkuu, Fred Felix Minziro.

"Mechi yetu itachezwa CCM Kirumba saa 10:00 jioni, ninachoweza kusema Geita Gold tumeandaa timu kwa ajili ya kuleta ushindani, hata kama huko nyuma tulipoteza dhidi ya  Simba au Yanga, lakini hatukupoteza kirahisi, tulileta ushindani mkubwa, tunaamini tutapata matokeo na tutakuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga na kuzima ile rekodi yao ya kuwa timu isiyofungwa," alisema Liberatus.

Yanga ipo kileleni ikiongoza ligi kwa pointi 17, na ikishinda mechi hiyo itafikisha pointi 20 na kuzidi kukwea kileleni, wakati Geita Gold kama itafanikiwa kushinda, mbali ya kuzima rekodi ya Yanga kucheza mechi ya 45 bila kupoteza, itakuwa imefikisha jumla ya pointi 16 na kukwea hadi kwenye nafasi ya pili ya msimamo.Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema kuwa timu ya Geita Gold imeimarika kwa siku za karibuni na tangu msimu uliopita mechi yetu dhidi ya timu hiyo haikuwahi kuwa rahisi.

Itakuwa ngumu ya kutumia nguvu, lakini tumejiandaa kisaikolojia kuingia kwenye mchezo huo ili kusaka pointi tatu.

Ni rekodi nzuri, lakini siyo namba ya michezo, unaweza usifungwe lakini usifikishe malengo, malengo ni kutwaa ubingwa na siyo kumaliza bila kufungwa.

Amesema kuwa mbali na Mwamnyeto, pia Khalid Aucho hawatokuwepo.

Kocha wa Geita Gold Mathias Wandiba amesema wamejiandaa kikamilifu, wanaheshimu ubora wa Yanga, lakini timu yao pia ina wachezaji bora, tunajua tunakwenda kucheza mechi muhimu, tutahakikisha tunashinda, tupo nyumbani, hatuhitaji kupoteza, kikubwa tumejiandaa kwa mchezo huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live