Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yashtuka, Chama, Dube, Baleke waondolewa!

Chama X Dube Balekee Yanga yashtuka, Chama, Dube, Baleke waondolewa!

Mon, 15 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga ni kama imeshtuka vile. Baada ya kuiona Simba ipo kambini Ismailia, Misri na kusikia Azam FC nayo imeondoka nchini kwenda Morocco kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao, nao fasta wameamua kufanya jambo.

Mabosi wa klabu hiyo wakishirikiana na kocha Miguel Gamondi, wameamua kuwaondoa mastaa wa timu hiyo akiwamo Jean Baleke, Clatous Chama na Prince Dube jijini Dar es Salaam na kuwapeleka nje ya nchi ili kujifua kabla ya kuja kuliamsha kwa msimu ujao wa mashindano wakianza na Ngao ya Jamii.

Hivi unavyosoma ni kwamba, Yanga imebakiza siku mbili tu kabla ya kupaa kwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki zaidi ya mbili na kucheza mechi kadhaa za kimataifa kujiweka fiti, ikifuta mpango wa awali wa kujichimbia Avic Kigamboni kama ilivyofanya misimu miwili mfululizo iliyopita.

Uhakika kwa sasa ni kwamba Yanga itaenda kukaa Afrika Kusini kwa siku zisizopungua 18 kujindaa na msimu mpya sambamba na kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kimataifa huko Afrika Kusini, ikiwamo mechi maalumu ya michuano ya Kombe la Toyota.

Hesabu mpya za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata na kujiridhisha ni kwamba,Yanga itaondoka nchini Julai 17 ikiunganisha na mualiko iliyopewa na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, itakayocheza nayo mechi maalum iliyoandaliwa na kampuni ya magari ya Toyota.

Kabla ya mchezo huo, Yanga itajificha katika jiji moja ambalo tayari Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said ameshajiridhisha kuwa, timu itakuwa salama kwa siku zote maandalizi hayo.

Hivi unavyosoma Mwanaspoti ni lazima ujue kuwa, Hersi yuko Afrika Kusini kwa mapumziko na shughuli zingine binafsi akikutana na mabosi mbalimbali wa soka nchini humo na ndipo ilipozaliwa mipango ya timu kupelekewa huko kujifua kama ilivyo kwa Simba na Azam zilizokilimbilia Kaskazini mwa Afrika.

Inaelezwa kuwa, Yanga ikiwa huko itacheza mechi mbili au tatu za kirafiki katika kambi hiyo itakayotumia na tayari mbili katyi ya hizo zimeshajulikana kuwa, itacheza dhidi Kaizer Chiefs na Augsburg ya Ujerumani huku mchezo mmoja ukiwa bado haujawekwa wazi.

Baada ya mechi hizo, kikosi cha Yanga kilichoongezewa nguvu ya kusajiliwa Clatous Chama, Prince Dube, Jean Baleke, Chadrack Boka, Aziz Andambwile na kipa Abubakar Khomeiny inaweza kurejea nchini Agosti 2 ikiwa tayari kwa Tamasha la Wiki ya Mwananchi litakalofanyika Agosti 4 Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ingawa hakutaka kuweka wazi ratiba hizo nzima, lakini amelithibitishia Mwanaspoti kuwa watakuwa na takribani wiki hizo mbili nje ya Tanzania katika kujipanga sawasawa.

"Tunaweza kukaa hapa Avic na kujipanga na kila kitu, lakini kuna wakati unaweza kuwa na utaratibu tofauti, nadhani tunaweza kutoka nje ya Tanzania kwa kama wiki mbili ili tupate utulivu zaidi," alisema Gamondi na kuongeza;

"Tunataka kuwa tayari kwa msimu ujao mapema, tutakuwa na ratiba ngumu ya kutetea mafanikio yetu ya msimu uliopita lakini pia malengo mengine ya kufika mbali ambayo tumejiwekea."

Awali Yanga ilikuwa inafikiria kuweka kambi, Russia ilikopata mualiko, lakini kutokana na ufinyu wa muda ikabadilisha uamuzi wake na kuamua kukimbilia Afrika Kusini.

Hii inakuwa mara ya pili kwa Yanga kuweka kambi nje ya Tanzania ndani ya misimu mitatu ambapo mapema ikiwa inataka kujiandaa msimu wa 2021/22 iliweka kambi fupi Morocco kisha kukatisha kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19.

Baada ya kambi hiyo ya Moroco, Yanga haikuwa na utaratibu wa kuweka kambi nje ya nchi ikiamua kujichimbia Avic Town kisha ikachukua mataji ikitokea hapo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: