Ushindi wa jumla ya mabao 7-2 ambao Yanga iliupata katika michezo miwili ya Dabi dhidi ya Simba msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara umeshangiliwa upya katika mkutano mkuu wa mwaka wa klabu hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea wakati wa hotuba ya rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said ambapo alikuwa akiongelea mafanikio waliyoyapata msimu wa 2023-24 kwa kutwaa ubingwa wa 30 Ligi Kuu Bara.
Ndipo Rais huyo akakatishwa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe baada ya kuyaingiza makombe iliyotwaa msimu huu ukumbini hapo kwa kuwakumbusha kupitia skrini kubwa namna ilivyokuwa kwa kuonyesha mabao yote wakati wakiifunga Simba kwenye Uwanja wa Mkapa.
Ndipo shangwe lilipoibuka kwa wenyekiti wa matawi wa klabu hiyo kwa kushangilia upya mabao ambayo walipata katika michezo hiyo miwili wa kwanza iliyoshinda mabao 5-1 na ule wa pili ilitamba kwa mabao 2-1.
Kamwe hakuishia hapo, aliendelea kuchombeza kwa kuonyesha mabango ambayo waliyaweka katika maeneo mbalimbali huku akihitimisha kwa kuonyesha mashabiki wa timu hiyo walivyokunywa supu.
Baada ya hayo ndipo Hersi alipoendelea kwa kuongelea pia mafanikio ya upande wa Shirikisho (FA) kwa kuifunga Azam FC katika mchezo wa fainali Zanzibar.
Kombe hilo nalo liliingizwa ukumbini hapo huku ukishangiliwa kama ilivyokuwa ule wa Ligi Kuu Bara na mabao muhimu yaliyowafanya watambe yakionyeshwa katika skrini hiyo kubwa.
Kiongozi huyo wa juu wa klabu hiyo, alieleza pia mafanikio waliyoyapata ni upande wa kimataifa kwa kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika walipoondolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.