Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yasaka rekodi ya 3 Ahly

Yanga Bilioni 2 CAF Yanga yasaka rekodi ya 3 Ahly

Wed, 28 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job amesema wanaenda Cairo kusaka rekodi ya tatu kwa kuhakikisha wanaongoza kundi ili kupata faida ya kuanzia ugenini hatua ya robo fainali.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema wataingia kwenye mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani wao lakini wakiwa wamejiandaa vizuri ili kuonyesha ushindani, lengo lao likiwa ni kusaka nafasi ya kuongoza kundi.

“Kuna faida tukiongoza kundi, tunapata nafasi ya kuanzia ugenini na kurudi kumaliza nyumbani, pia tutakuwa tumeandika rekodi nyingine kitu ambacho tunakihitaji,” alisema Job.

“Tulianza na makundi Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25, robo fainali sasa tunasaka rekodi ya kuongoza kundi ambayo pia itakuwa na faida kwentu,” alisema.

Kwa mujibu wa CAF katika droo ya robo fainali, vinara wa makundi yote manne watapangwa kucheza dhidi ya timu ambazo zilizoshika nafasi ya pili kwenye makundi mengine, wababe hao wanne wataanzia ugenini kwenye michezo ya robo fainali ya kwanza huku wakimalizia nyumbani.

Timu kutoka kundi moja haziwezi kukutana katika hatua ya robo fainali pamoja na zile ambazo zimetoka nchi moja kama vile Simba na Yanga.

Pia nahodha huyo alisisitiza haijaisha hadi iishe, bado wana dakika nyingine 90 ugenini dhidi ya Al Ahly ambayo amekiri haitakuwa rahisi watapambana kuhakikisha wanapata matokeo kuendeleza furaha.

Yanga Ijumaa itakuwa ugenini kuvaana na Al Ahly mchezo wa mwisho hatua ya makundi wakikutana na timu ambayo pia imefuzu hatua ya robo fainali.

“Ingekuwa tumeshamaliza kazi basi huo mchezo usingekuwepo ratiba inaonyesha tuna dakika nyingine 90 ngumu za kupambania timu kupata matokeo, hivyo tunaomba sapoti ya mashabiki iendelee, wapambanaji wao bado tunakazi ya kufanya;

“Napongeza namna walivyoisherehesha Pacome Day, wametutia moyo hadi sisi wachezaji kujipa matumaini na kuipambania timu kuweza kufikia malengo hivyo tunaahidi kuto kuwaangusha tunawategemea kama wao wanavyotutegemea.” alisema.

Job alisema haijaisha hadi iishe wanaenda kupambania pointi nyingine tatu muhimu dhidi ya Al Ahly ugenini huku akikiri hawatarajii mteremko, wanaenda kusaka heshima na kuendeleza furaha ya wananchi.

Ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kikosi cha wachezaji 24 kimeondoka nchini jana kikiongozana na benchi na viongozi wa klabu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) 36.

“Msafara wa watu 60, wachezaji 24 ndio wataondoka kwa ajili ya mchezo, benchi la ufundi 13 na viongozi kuanzia rais, watendaji wa timu, Makamu wa rais wa TFF jumla watakuwa 23.

“Tunaenda kutafuta furaha nyingine ya watanzania nchini Misri mchezo utachezwa saa moja usiku Ijumaa,” alisema Kamwe.

MASHABIKI ELFU 30 KUSHUHUDIA

Vyanzo vya habari Misri, vimefichua Al Ahly imeruhusiwa kuingiza mashabiki 30,000 kwenye mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Cairo, Misri.

Vyanzo vilifichua African Giants wamepata kibali kutoka kwa mamlaka ya usalama kuruhusu idadi hiyo kuhudhuria mechi hiyo ambayo inazikutanisha timu zote zikiwa zimeshafuzu robo fainali ya michuano hiyo.

Al Ahly ilitinga robo fainali baada ya kuifunga Medeama bao 1-0 huku Yanga ikifanya hivyo kwa kuichapa CR Belouizdad mabao 4-0 katika mechi za raundi ya tano.

Al Ahly inahitaji hata sare katika mechi hiyo ili kujikita kileleni mwa kundi hilo.

Chanzo: Mwanaspoti