Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yasaka rekodi mpya

Yanga Dar Es Salaam Mastaa wa Kikosi cha Yanga

Sat, 20 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga walitua jana alfajiri, huku Kocha Nasreddine Nabi akizuia shangwe kwenye mapokezi ya timu hiyo akitaka hadi wakamalizane kwanza na Singida Big Stars katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) inayopigwa Jumapili.

Yanga inatarajiwa kuunga safari hadi Dodoma kabla ya kusafiri kwa basi hadi Singida kwa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Liti, mkoani Singida, huku mabosi wa klabu hiyo wakipiga hesabu za kubeba ubingwa wa Afrika ili kuandika rekodi mpya itakayochukua muda mrefu kufikiwa tena.

Yanga imetinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya juzi kuitungua 2-1 na mchezo wa awali nyumbani kuichapa 2-0 jana asubuhi ilianza safari kutoka Johannesburg kabla ya usiku kutua Ethiopia la alfajiri ya leo ilitarajiwa kutua kutoka Sauzi kisha wachezaji kupewa mapumziko ya siku moja kabla ya kesho kuunga safari ya Singida, huku Nabi akizuia nyota kusherebuka.

"Kocha amesema hataki sherehe zozote kwa sasa, kwani amewaambia mastaa kazi haijaisha kwa kuwa wana mchezo mgumu dhidi ya Singida Big Stars kabla ya kuanza jukumu la fainali ya CAF," kilisema chanzo kutoka ndani ya Yanga wakati wakiwa njiani kurejea nchini.

Inaelezwa Nabi hataki wachezaji wazinguliwe kwa sasa wakati mipango yao ni kuona inaweka akili zaidi kwenye nusu fainali hiyo ya ASFC ikitetea taji kwa msimu wa pili mfululizo na pia kuona inafanya vyema kwenye mechi mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikianzia nyumbani.

Licha ya Nabi kuzuia shangwe hizo, lakini mashabiki wa Yanga walipanga kuamkia Uwanja wa Ndege ili kuwapokea mashujaa ambao ambao wameandika historia ya kuwa timu ya kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kutinga fainali ya Shirikisho Afrika tangu michuano iliyobadilishwa upya 2004.

MABOSI WAJIPANGA

Mabosi wa Yanga ni kama wamenogewa kwani awali walipoanza michuano walipanga kufika mbali ili kuzima kelele za watani wao na ghafla ikajikuta nusu fainali na juzi ikavuka hadi fainali na fasta wakabadili mawazo wakitaka kubeba kabisa ndoo ili kuandika historia mpya.

Rais wa Yanga, Injinia Hersi alisema, malengo yao kwa msimu huu katika Kombe la Shirikisho waliyapita kitambo lakini kutokana na ubora wa kikosi chao na kazi kubwa wanayofanya, sasa wamejipa lengo jingine jipya ambalo ni kuhakikisha wanabeba ubingwa.

Hersi aliwapongeza wachezaji wa Yanga, benchi la ufundi, uongozi na mashabiki kwa kufanikisha hilo huku akiwataka kukaza buti hadi wachukue ubingwa akiamini inawezekana.

“Ni historia tumeweka katika soka kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, hakuna timu ya Tanzania iliyowahi kufika hatua hii katika michuano hii ila sisi tumefika fainali. Nawapongeza wote waliohusika kuhakikisha tunafika hapa lakini pia hatupaswi kuishia hapa tunatakiwa kuhakikisha tunalibeba kombe hili na kuweka rekodi bora zaidi,” alisema Hersi na kuongeza;

“Huenda kuna watu hawaamini, sasa inabidi tubebe Kombe ili washangae zaidi, kwa timu tuliyonayo hilo linawezekana na tupo tayari.”

Baada ya hapo itaanza mipango ya mechi mbili za ligi kumalizia msimu lakini kubwa zaidi itakuwa ni mipango ya mechi mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ikiialika Kwa Mkapa Mei 28 kisha kurudiana nao mjini Algers Juni 3 na mshindi wa jumla kubeba taji hilo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: