Klabu ya Yanga imefanikiwa kutinfa hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitungua timu ya ASAS FC ya Djibouti kwa bao 5-1 katika mchezo wa pili wa marudiano ulipigwa leo Jumamosi, Agosti 26, 2023 karika Dimba la Azam Complex pale Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yamwefungwa na Maxi Mpia Nzengeli ambaye amefunga mabao mawili, la kwanza dakika ya 7 na bao la tano dakika ya 90+2. Mabao mengine yamefungwa na Hafiz Wantah Konkoni dakika ya 44, Pacome Zouzoua dakika ya 55 na Clement Waridi Mzize dakika ya 69.
Bao pekee la kufutia machozi la Asas Fc limefungwa na Mayor dakika ya 85 kwa mkwaju wa penati baada ya Zawadi Mauya kufanya madhambi ndani ya boksi la timu yake.
Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya pili ya mtoano kwa jumla ya bao 7-1 dhidi ya Asas kwani hapo awali kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Jumamosi iliyopita, Wananchi walishinda kwa bao 2-0.
Kipigo cha leo cha bao tano kinakuja ikiwa ni siku mbili baada ya Yanga kuichapa KMC bao 5-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika dimba hilo hilo la Chamazi.
Aidha, Yanga watakutana sasa na Al-Merreikh ya Sudan ambayo nayo imefanikiwa kutinga hatua inayofuata kwa kuitoa Otoho D'Oyo FC ya nchini Congo Brazzaville jana.
Katika mchezo dhidi ya Merreikh, Yanga wataanzia ugenini katika mchezo wa kwanza kwani wenyeji wao wamechagua mechi zao za nyumbani zitachezwa nchini Rwanda kutokana na machafuko yanayoendelea Sudan kwa sasa.