Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yapiga mtu 6-1, JKT Queens chupuchupu

Yanga Princes 6 Yanga yapiga mtu 6-1, JKT Queens chupuchupu

Thu, 28 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu ya Wanawake Bara imeendelea leo kwa mechi za mzunguko wa pili kupigwa, huku Yanga Princess ikiendeleza vichapo kwa wapinzani wake ambapo imeinyuka Amani Queens ya Lindi kwa mabao 6-1.

Yanga Princess imepata ushindi huo katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kupaa katika kilele cha msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi sita na faida ya mabao saba.

Mabao ya Yanga Princess yamefungwa na Janeth Bundi na Precious Christopher ambao wote wamefunga mawili mawili kila mmoja, huku mengine yakifungwa na Noela Luhala na Madina Traole, ilhali bao pekee la Amani Queen likifungwa na Janeth Nyagali.

Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Yanga ambayo ilianza ligi kwa kuinyuka Baobab Queens ya Dodoma mabao 2-0, huku Amani Queens ikicheza kwa mara ya kwanza baada ya mchezo dhidi ya Fountain Gate kuahirishwa kutokana na timu hiyo kukosa nauli ya kwenda Dodoma.

Mabingwa watetezi, JKT Queens leo nusura wapunguzwe kasi na Geita Gold, lakini bao la dakika ya 88 la Johari Hamis limewaokoa na kuondoka na ushindi wa 1-0 katika Uwanja wa Nyankumbu, Geita. Ni ushindi wa pili mfululizo ikianza kwa kuichapa Bunda Queens 4-0.

Nayo Fountain Gate Princess ya Dodoma imetakata nyumbani katika Uwanja wa Jamhuri kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ceassia ya Iringa. Mchezo huo ni wa kwanza kwa wenyeji baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya Amani Queens kuahirishwa.

Mabao ya Fountain Gate yamefungwa na mshambuliaji Amina Ramadhan aliyetupia mawili na Husnath Ubamba, huku yale ya Ceassia yakiwekwa kambani na Janeth Matulanga na Stella Wilbert. Hicho ni kipigo cha pili kwa Ceassia Queens baada ya kufungwa mabao 5-0 na Simba Queens.

Bunda Queens ya Mara imeendelea kuchechemea katika ligi hiyo baada ya leo kupokea kipigo cha pili mfululizo nyumbani katika Uwanja wa Karume, Musoma kwa kufungwa mabao 3-2 na Alliance Girls ya Mwanza. Bunda ambayo ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu ilianza vibaya kwa kufungwa mabao 4-0 na mabingwa watetezi, JKT Queens.

Ligi hiyo itaendelea kesho wenyeji Simba Queens wataikaribisha Baobab Queens ya Dodoma katika Uwanja wa Azam Complex ambapo Simba ilianza kwa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Ceassia huku Baobab ikipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga Princess.

Chanzo: Mwanaspoti