Klabu ya Yanga itaondokewa na nyota wake wa kimataifa ambao wamepata nafasi ya kuitwa katika majukumu ya timu za taifa, hasa wale wachezaji ambao wanaingia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Yanga itakosa huduma ya wachezaji hao baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji mtanange utakaopigwa dimba la Benjamin Mkapa wiki hii.
Wachezaji ambao wanang’oka Timu ya Wananchi kwenda kwenye majukumu ya timu ya taifa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Bingwa Afrika AFCON 2022 ni Yanick Bangala, Mukoko Tunombe na Djuma Shabani.
Habari njema kwa Yanga ni kuwa timu hiyo itaenda Visiwani Zanzibar kwenye majukumu ya Kombe la Mapinduzi kuanzia Januari 2.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema nyota hao hawatafuatana na wenzao kwenda Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi ingawa mechi yao na Dodoma Jiji watakuwepo.
Alisema kwenye eneo la kiungo cha ulinzi ambapo watakosekana Mukoko na Bangala, wanategemea kumtumia Zawadi Mauya na kuongeza nyota wengine kutoka kikosi B.
Alisema mbali na nyota hao watatu pia wanatarajia kumkosa kipa wao namba moja Djigui Diarra ambaye ataungana na timu yake ya taifa ya Mali hivyo watakuwa na kipa Erick Johora sambamba na kipa kutoka kikosi B huku timu ikipambana kusaka kipa mwingine.