Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yapata hasara, yaanika usajili na mishahara ya kina Pacome, KI 2023/2024

Yanga Hasara Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu ya Yanga SC imepata hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni kwa mujibu wa ripoti yake ya mapato na matumizi kwa msimu wa 2023/2024.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa jana katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Yanga uliofanyika kwenye Ukumbi wa JKNICC ilionyesha kwamba Yanga ilipata mapato ya jumla ya Sh21.19 bilioni lakini matumizi yalikuwa ni Sh.22.29, hivyo kuingiza hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Usajili na uhamisho wa wachezaji kama kina Pacome Zouzoua, Yao Kouassi, Joseph Guede ni moja ya maeneo yaliyotumia fedha nyingi, ambapo Sh3.5 bilioni zilitumika kuhakikisha klabu inapata wachezaji bora.

Gharama za mishahara kwa wachezaji na benchi la ufundi zilitumia sehemu kubwa zaidi ya bajeti, ikifikia Sh7.39 bilioni. Hii inaonyesha nia ya klabu kuboresha viwango vya wachezaji na kuhakikisha wanapata maslahi bora.

Matumizi mengine muhimu ni pamoja na usafiri, chakula na malazi, ambapo klabu ilitumia Sh 2.89 bilioni kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanapata huduma bora wakati wa safari na kambi za mazoezi. Maandalizi ya mechi nayo yaligharimu Sh 1.85 bilioni, fedha hizi zikiwa zimeelekezwa katika kuhakikisha vifaa na maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi yanakamilika kwa wakati.

Motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi imechukua Sh 2.6 bilioni, fedha hizi zikiwa ni kwa ajili ya bonasi na zawadi kwa wachezaji na makocha kutokana na mafanikio mbalimbali. Gharama za kambi zimesimama kwenye Sh702 milioni, huku 'compliance' ikigharimu Sh944 milioni. Gharama za kiutawala zimefikia Sh 1.46 bilioni, ikijumuisha matumizi ya ofisi na mishahara ya wafanyakazi wa utawala.

Aidha, Yanga imetumia Sh424 milioni kwa ajili ya masoko na Sh503 milioni kwa gharama za kifedha, ambazo ni pamoja na riba za mikopo na huduma za kibenki. Jumla ya matumizi yote kwa msimu huu yamefikia Sh22.29 bilioni.

Ripoti hii inaonyesha jinsi klabu imekuwa ikijitahidi kuboresha miundombinu na ustawi wa wachezaji wake kupitia matumizi bora ya fedha. Kwa uwazi huu, Yanga SC inatarajia kuendelea kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanachama na wadau mbalimbali ili kuleta mafanikio zaidi katika msimu ujao.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: