Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yapania kulipa kisasi Nigeria

GODSWILL Yanga yapania kulipa kisasi Nigeria

Sun, 23 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Zamu yenu sasa! Ndio kauli ya kibabe ambayo Yanga inawatambia wenyeji wao Rivers United katika mchezo wa kwanza leo wa hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa katika Uwanja wa Yakubu Gowon jijini Port Harcourt kuanzia saa 10:00 jioni.

Yanga inaamini ni zamu imefika sasa kwa Rivers United kuonja machungu kama ambayo wao walikutana nayo dhidi yao katika msimu uliopita ambao timu hiyo ya Nigeria iliwatupa nje katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0 ikiwafunga bao 1-0 nyumbani na ugenini.

"Tupo vyema hapa Nigeria na tayari tumeshafika katika mji ambao mechi hii itachezwa. Malengo yetu ni kufanya vizuri katika mechi hii kwa kupata matokeo ambayo yatatufanya tusiwe na kazi kubwa katika mechi ya nyumbani," alitamba Ofisa Habari wa Yanga Ally Kamwe.

Ushindi katika mechi hiyo sio tu utaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali bali pia kumaliza unyonge katika ardhi ya Nigeria kwani hapo kabla iliwahi kucheza mechi mbili nchini humo bila kupata ushindi, ikifungwa na Rivers United lakini pia imewahi kutoka sare na Enugu Rangers. Vita ya mbinu

Silaha kubwa ya Nasreddine Nabi ni umiliki wa mpira hasa katikati mwa uwanja kwa pasi za taratibu ambazo hupelekwa pembezoni mwa uwanja kwa mawinga au mabeki wa kushoto na kulia ambao huwa na jukumu la kupiga krosi au pasi za mwisho kwenda kwa washambuliaji.

Msanifu wa mbinu hiyo ya Nabi ni kiungo Khalid Aucho ambaye amekuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi sahihi kwenda kwa wahusika ambao mara nyingi huwa ni winga Ducapel Moloko au beki wa kushoto, Joyce Lomalisa.

Hata hivyo Yanga wanapaswa kuwa makini sana na mbinu ya Rivers United kukaba kuanzia katika mstari wa mbele kwani wanaweza kujikuta wakifanya makosa yanayoweza kuwapa faida wapinzani wao ambao ndio wamekuwa wakiitumia kuwanyima uhuru walinzi wa timu pinzani kumiliki mpira na kuanza kujenga mashambulizi. Takwimu zinatia moyo

Yanga hawaingii kinyonge katika mechi ya leo kwani kwa ubora wa siku za hivi karibuni, wameonekana kuwazidi Rivers United na matokeo ya mechi tano zilizopita kwa kila timu kwenye mashindano tofauti yanaweza kuwa shahidi wa hilo.

Wakati Yanga ikipoteza mechi moja tu kati ya tano zilizopita huku ikipata ushindi mara nne, Rivers United yenyewe imeshinda mechi moja tu, ikitoka sare mbili na kupoteza michezo miwili.

Katika michezo 10 iliyopita ya mashindano ya klabu Afrika ambayo Rivers United walicheza wakiwa nyumbani, wameibuka na ushindi mara nane na kutoka sare mbili huku wakifunga mabao 33 sawa na wastani wa mabao 3.3 kwa mecghi huku wakiwa wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara sita tu.

Wageni Yanga nao wamekuwa wakijitutumua ugenini katika mashindano ya kimataifa na kudhihirisha hilo, katika michezo 10 iliyopita ya mashindano hayo ambayo walicheza ugenini hivi karibuni, wameibuka na ushindi mara nne, wametoka sare moja na kupoteza michezo mitano, wamefunga mabao tisa na wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara 10.

Mayele, Musonda wabeba lawama

Matumaini makubwa kwa Yanga yanapaswa kuelekezwa kwa washambuliaji wake wawili, Fiston Mayele na Kennedy Musonda kutokana na kiwango bora cha kufumania nyavu na kutengeneza mabao walichokionyesha katika mechi za hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Mayele amefunga mabao matatu katika mashindano hayo na kupiga pasi moja ya mwisho wakati Musonda yeye amefunga mabao mawili na kupiga tatu za mabao.

Kwenye eneo la kiungo, Yanga itakuwa inategemea zaidi kazi ya Mudathir Yahya ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali kwa kuilinda vyema safu ya ulinzi lakinin kuisukuma timu mbele.

Yanga inapaswa kumchunga zaidi nyota wa Rivers United, Paul Acquah ambaye ndio kinara wa kufumania nyavu katika mashindano hayo akipachika mabao manne.

Chanzo: Mwanaspoti