Baada ya kucheza mechi nne mfululizo bila kupata ushindi, timu ya vijana ya Yanga (u-20), juzi ilishinda kwa mabao 3-2 mbele ya Tanzania Prisons U-20, katika mwendelezo wa Ligi ya Vijana huku vikosi vya vijana wa Dodoma Jiji na Coastal Union vikiwa havishikiki.
Ligi hiyo inayohusisha vikosi 16 vya vijana kutoka timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu inachezwa kwa mfumo wa makundi mawili A na B na sasa imefika mzunguko wa sita.
Kundi A lenye timu nane linaongozwa na Coastal yenye alama 12, ikifuatia Azam iliye na alama 11, Namungo ikiwa nazo nane timu zote hizo zikiwa zimecheza mechi sita kila moja huku Prisons, Yanga, KMC, Simba zikifuata zikiwa zimecheza mechi tano kila moja na Ihefu ikiwa mkiani baada ya mechi nne.
Kundi B timu zote zimecheza mechi sita, linaongozwa na Dodoma yenye alama 15, ikifuatiwa na Mtibwa yenye 13, Mashujaa ikiwa nafasi ya taqtu na pointi tisa, ikifuatia Singida Fountain Gate yenye nane sawa na JKT Tanzania. Geita Gold ipo nafasi ya sita na alama saba, Kagera ikiwa ya saba na alama tano huku Tabora United ikiburuza mkia na pointi mbili.
Ushindi ilioupata Yanga juzi umeifanya Tabora kusalia kuwa timu pekee ambayo haijashinda mechi yoyote hadi sasa.
Timu zitakazomaliza nafasi nne za juu kwenye kila kundi zitatinga hatua ya nane bora na kucheza mtoano kisha nusu fainali na baadaye fainali atakapopatikana bingwa wa mashindano hayo kwa msimu huu.