Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaongoza kwa mashabiki, Simba yapiga mkwanja mrefu

Aziz Che Malone Nstagram Yanga yaongoza kwa mashabiki, Simba yapiga mkwanja mrefu

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Yanga imeongoza kwa kuingiza mashabiki wengi kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, huku watani zao wa jadi, Simba wao wakiwa vinara wa mapato viwanjani kwa msimu wa 2023/24.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotokea jana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), JKT Tanzania ndiyo timu iliyopata mapato kiduchu zaidi, huku Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja, ikiingiza mashabiki wachache zaidi kati ya timu zote 16 zilizoshiriki Ligi Kuu msimu uliopita.

Takwimu zinaonyesha kuwa Yanga imeongoza, ikiingiza jumla ya mashabiki 141,911 kwa msimu, ikifuatiwa na Simba ambayo iliingiza mashabiki 112, 717.

Timu ya Mashujaa FC, yenye maskani yake mjini Kigoma, imeshika nafasi ya tatu, ikiingiza mashabiki 45,638, huku Tabora United ikiwa nafasi ya nne, ikikusanya 43,808 na Azam FC, imekuwa ya tano ikiingiza jumla ya mashabiki 35,379.

Kwa mujibu wa takwimu hizo za TFF, nafasi ya sita imechukuliwa na Dodoma Jiji, yenyewe ikiwa na mashabiki 30,381, Geita Gold ambayo imeshuka daraja, ikiwa ya saba, ikiingiza 24,774, Coastal Union ikikamata nafasi ya nane, mashabiki wake ni 24,161, maafande wa Prisons wakiwa kwenye nafasi ya tisa, wakiwa na mashabiki 24,147, na nafasi ya 10 imeenda kwa Singida Fountain Gate, ambayo kwa msimu mzima imeingiza mashabiki 21,154.

Mtibwa Sugar ni ya mwisho, ikiingiza mashabiki 7,529, ambayo ndiyo walioingia Uwanja wa Manungu Complex, kutazama mechi za Ligi Kuu msimu uliopita.

Simba imeingiza kiasi cha Sh. 835,805,000 na kuwa kinara wa mapato kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika, ikifuatiwa na Yanga ambayo imeingiza Sh. 825,065,000 kwa msimu mzima wa ligi hiyo.

Tabora United imekamata nafasi ya tatu kwa wingi wa mapato, ikikusanya Sh. 223,270,000, wakati Mashujaa FC, ikiwa nafasi ya nne, ikiingiza Sh. 140,702, 000.

Singida United, iko nafasi ya tano, yenyewe ikiingiza Sh. 135, 045,000 na namba sita inashikiliwa na Dodoma Jiji ambayo imekusanya Sh. 126,722,000, Geita Gold ambayo imeteremka daraja, ikivuna Sh. 119,046,000 na imeshika nafasi ya saba, Prisons iko nafasi ya nane na Sh. 118, 835,000 zake, wakati Azam FC imekamata nafasi ya tisa, ikiingiza kiasi cha Sh. 116,048,000 na nafasi ya kumi imetwaliwa na Costal Union, ikiingiza Sh. 102, 509,000.

Timu ya JKT Tanzania imepata pesa kiduchu msimu uliopita, ikiambuliwa Sh. 32,054,000 za mapato yao yote ya mlangoni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live