Uongozi wa Klabu ya Yanga umesema upo makini katika mchakato wa kusaka kocha Mkuu na wameweka malengo ya kumpata kocha mwenye uwezo mkubwa na aliyefanikiwa kupata mataji Afrika.
Yanga ipo kwenye mchakato wa kusaka kocha mpya baada ya aliyekuwa kocha wao Nasreddine Nabi kugoma kuongeza mkataba mpya na anatajwa kujiunga na klabu ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Habari na klabu hiyo, Ali Kamwe amesema kitu cha kwanza wanachoangalia ni uwezo wa kocha na mataji ambayo amefanikiwa kuyapata akiwa na klabu nyingine.
"Sifa zipo nyingi za kocha anayetakiwa na Yanga, lakini namba moja ni mwenye mataji, nawaambia makocha wote ambao wametuma CV, kama hawana mataji kwenye klabu walizitoka, angalau moja tu, we soma Uefa, Class A, B, D mpaka F, Q hadi Z, kama huna mataji hapana, kwa sababu sisi ni timu ya kunyanyua makwapa karibuni kila msimu," alisema Kamwe.
Ofisa Habari huyo hakukanusha wala kukataa kwamba makocha wawili wakubwa Afrika, Mkongomani Florent Ibenge na Msauzi Afrika, Pitso Mosimane kutuma maombi yao kwenye klabu hiyo.
"Ukizungumza mmoja wa makocha wenye mataji ni Ibenge, alichukua Kombe la Shirikisho akiwa na RS Berkane ya Morocco, Mosimane, kafanya vizuri akiwa na Mamelodi Sundowns pale Afrika Kusini, kafanya vyema akiwa na Al Ahly kule Misri, ni mwenye mafanikio na mataji.
"Kama watu wanaihusisha Yanga na makocha hao ni kwamba wameshajua kuwa tunahitaji makocha wenye mataji, baada ya Nabi kuondoka makocha wengi wametuma CV, hii inaonyesha kuwa Yanga ni timu ambayo kwa sasa inafuatiliwa sana Afrika," alisema.
Alisema bado wapo kwenye mchakato wa kumpata kocha mkuu wa Yanga na mashabiki waendelee kuwa watulivu watatangaziwa kocha mpya.
Hata hivyo, taarifa zinasema Ibenge ndiye ambaye anapewa nafasi kubwa kumrithi Nabi, wengine wanaohusishwa ni Juan Carlos Garrrido kutoka Hispania, Watunisia Fouuzi Benzarti, Nabil Maaloul na Julien Chevalier kutoka Ufaransa.