CEO wa Klabu ya Yanga SC, Andre Mtine juzi amemuandikia barua kiungo wa klabu hiyo aliyeko kwenye mgogoro wa kimkataba Feisali Salum, akimtaka kurejea kambini haraka kujiunga na wenzake kwenye maandalizi ya mashindano mbalimbali.
Mtine amemtaka Feisali kuheshimu mkataba baina yake na klabu ya Yanga uliosainiwa tarehe 10/Agosti/2020 na kutarajiwa kumalizika Mei 30, 2024.
Amemtaka kuheshimu mkataba kama ilivyoainishwa kwenye kipengele cha 8 na kuripoti kambini baada ya hukumu ya kamati ya sheria, hadhi na haki za wachezaji na wanachama inayoongozwa na Mweyekiti Said Sudi.
Mtine ameeleza nia ya Yanga SC kutaka kumtumia kiungo huyo wa Kizanzibar kwenye mashindano mbalimbali ya ndani na nje ambayo Yanga SC inashiriki, pia umuhimu wa yeye kwenye klabu ya Yanga SC.
"Mpaka sasa msimamo wa Feisal Salum ni ule ule, hayuko tayari kurejea Yanga ndio maana tumeomba marejeo tukiamini kamati inaweza kufanya maamuzi mengineyo ila kama maamuzi ya kamati yataendelea kusalia kama yalivyo sasa tutaenda mbele zaidi," amesema Nduruma Majembe, Wakili anaemsimamia Feisal.