Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yamfuata mwarabu kishua

Yanga Jezi 13 Yanga yamfuata mwarabu kishua

Sat, 4 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mechi sita za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, zinaipa uhakika Yanga kuvuna Sh 2.1 bilioni, lakini jambo la kufurahisha zaidi ni namna fedha hizo zinavyowapa jeuri vijana wa Jangwani katika mechi za ugenini wakianzia kwa Waarabu wa Tunisia, US Monastir.

Yanga itavaana na Monastir katika mechi ya Kundi D ya michuano hiyo Februari 12 kabla ya kurejea nyumbani kuvaana na TP Mazembe kisha kuifuata tena Real Bamako ya Mali.

Mkwanja huo mrefu Yanga unaweza kuongezeka kama itafika mbali zaidi katika michuano hiyo, inatokana na mkataba wa udhamini iliyoingia juzi na Kampuni ya Haier ukiwa na thamani ya Sh 1.5 bilioni na fedha walizojihakikishia kwa kucheza makundi ya Shirikisho Afrika kiasi cha Dola 275,000 (Sh 643 milioni) kutoka Caf.

Mkataba huo mpya umeibua sintofahamu kwa wadhamini wakuu wa klabu hiyo, SportPesa ambao wametishia kuwadai fidia kwa kukiuka makubaliano, japo mabosi wa Jangwani wamesema hilo linazungumzika na lengo la kuwasaka Haier ni kusaidia kujipunguzia gharama kwa mechi za CAF.

Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti, imegundua fedha hizo zinaipa jeuri Yanga kufanya maandalizi makubwa nje ya uwanja kwa mechi hizo hasa za ugenini ambazo huwa na changamoto barani Afrika hasa kwa maeneo ya usafiri, malazi, posho na huduma kama za chakula na matibabu.

Usafiri

Yanga itakuwa na mechi tatu ugenini katika nchi ambazo zina changamoto kubwa ya usafiri kutokana na kutokuwepo kwa ndege zinazokwenda moja kwa moja kutokea hapa Tanzania ambazo ni Tunisia, Mali na DR Congo.

Kwa mkwanja huo ambao Yanga itapata wakati ikishiriki hatua ya makundi unaipa jeuri ya kuweza kuingia katika nchi hizo na ndege za kukodi ambazo zitaenda moja kwa moja zikitokea Tanzania jambo ambalo litapunguza usumbufu na uchovu kwa msafara mzima.

Mwanaspoti linafahamu gharama ya ndege ya kukodi kwa safari moja kwenda katika miongoni mwa nchi hizo, haizidi Sh 300 milioni, hivyo kwa mechi tatu za ugenini, Yanga inaweza kutumia Sh 900 milioni kwa usafiri na hivyo kubakia na kiasi Sh 1.2 bilioni kwa ajili ya kutumika kwa mambo mengine.

Pia, hilo linaweza kuisaidia Yanga kwenda na kundi kubwa la watu wakiwemo mashabiki kwa ajili ya kusapoti katika mechi hizo dhidi ya US Monastir, Real Bamako na TP Mazembe.

Hoteli, malazi

Mara ya mwisho Yanga ilipokwenda Tunisia na kupata ushindi dhidi ya Club Africain ilifikia katika Hoteli ya kifahari ya Golden Carthage ambayo ina kumbi za mikutano, mabwawa ya kuogelea na huduma nyingine za kisasa.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, gharama ya chini ya chumba katika hoteli hiyo inaanzia kiasi cha Dola 100 kwa chumba huku ikiwa na gharama kubwa ya huduma za vyakula.

Katika Jiji la Bamako, gharama za hoteli za nyota tano, nyingi zinaanzia Sh 600,000 kwa chumba wakati kwa Lubumbashi iliko TP Mazembe kwa makadirio ya haraka ya chumba katika miongoni mwa hoteli za kifahari ni Dola 200.

Kwa mzigo ambao Yanga imeupata kupitia Haier na ule itakaovuna kutoka Caf, inaweza kwenda na msafara hata wa watu 80 katika nchi hizo na kuwagharamia hoteli pasipo kutingishika mfukoni.

Asikuambie mtu bwana, moja kati ya sababu zinazochangia timu kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa ni bonasi kubwa ya fedha ambazo wachezaji hupata iwapo timu imefanya vizuri.

Wakati Yanga inatamba ugenini dhidi ya Club Africain, kikosi hicho kiliahidiwa bonasi ya Sh 200 milioni na uongozi na wadau wa timu hiyo.

Katika hatua ya makundi ambayo imeingia, Yanga inaweza kutoa kiasi kama hicho au zaidi kwa mechi za ugenini na wasiwe na shaka kutokana na fungu kubwa ambalo inaingiza kutoka Caf na Haier.

Kila kitu fresh

Afisa Habari wa Yanga Kamwe, akikiri kila kitu kimeenda sawa na msafara utaondoka Dar es Salaam, Jumanne, huku nyota watakaoenda Tunisia wakifahamika mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara ya kesho dhidi ya Namungo.

“Michakato ya safari inaendelea na tupo katika hatua nzuri, tunatarajia kuondoka na kabla ya siku hiyo mtajulishwa msafara mzima,” alisema Kamwe.

Chanzo: Mwanaspoti