Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limeipiga faini ya Shilingi milioni 11 klabu ya Yanga baada ya kushindwa kujibu madai ya kuwafanyia fujo baadhi ya watu waliokuwa kwenye msafara wa Rivers United ya Nigeria.
Malalamiko hayo yametokana na mechi ya hatua ya awali iliyochezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam Septemba 12 na Yanga kupoteza kwa bao 1-0, ambapo kupitia mitandao ya kijamii ya timu hiyo walilalamika kupigwa kwa watu mbalimbali akiwemo Ofisa habari wa timu hiyo, Charles Mayuku.
Rivers United walipeleka malalamiko hayo CAF na kupitia mtandao wao wamethibitisha kupokea malalamiko hayo.
Pia CAF wamesema mechi hiyo haikutakiwa kuwepo mashabiki ila walibaini baadhi ya mashabiki uwanjani.
CAF ilituma malalamiko hayo kwa Yanga kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), na wamesema hakukuwa na mrejesho wowote kutoka kwenye Shirikisho hilo.
Kutokana na hilo bodi ya nidhamu imeipiga faini Yanga kiasi cha 5,000 USD sawa na Sh11 milioni za kitanzania.