Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaleyale Mapinduzi

91378 Mtibwa+pic Yanga yaleyale Mapinduzi

Fri, 10 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

YANGA usiku wa leo ikicheza kwa mara ya kwanza mbele ya kocha wao mpya, Luc Eymael imekumbana na kipigo cha mikwaju ya penalti na kung'oka kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ikiendeleza mwenendo mbaya kwenye michuano hiyo.

Yanga ilifungwa penalti 4-2 baada ya kuruhusu bao la jioni la kusawazisha la Mtibwa Sugar katika dakika 90 za pambano hilo la nusu fainali lililopigwa Uwanja wa Amaan.

Matokeo hayo hayakuonyesha kuwaumiza wana Yanga kwani walikuwa wakishangilia hata wakati watani zao wakiwakejeli wakiamini waliwakimbia kukutana nao kwenye fainali itakayopigwa Jumatatu, japo Msimbazi wanahitaji waifunge Azam kesho ndipo itinge fainali.

Yanga imefuzu fainali mara mbili tu kwenye michuano hiyo, ikiwamo ile ya kwanza mwaka 2007 walipobeba ubingwa kwa kuwafunga Mtibwa mabao 2-1 na mwaka 2011 walipochezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa watani wao Simba waliotwaa tyaji hilo mara tatu, nyuma ya Azam yenye rekodi ya kubeba mara tano.

Licha ya kucheza jihadi na hasa kipa Ramadhan Kabwili kufanya kazi kubwa ya kuokoa michomo ya nyota wa Mtibwa, bado Yanga iliruhusu bao sekunde chache kabla ya kumalizika kwa mchezo, ambao Eymaen alikuwa jukwani akichukua taarifa mbalimbali katika kipande cha katarasi.

Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza likifungwa kwa shuti kali la nje ya eneo la hatari mfungaji akiwa Deus Kaseke aliyepokea pasi safi ya kiungo Mapinduzi Balama na kumtungua kipa Said Mohammed 'Nduda' aliyejaribu kuupangua na kuusindikiza wavuni.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuwatoa Dante na Raphael waliopata maumivu nafasi zao zikachukuliwa na Kelvin Yondani na Abdulaziz Makame.

Dakika 48 Riphat alipoteza nafasi nzuri shuti lake dhaifu lilidakwa na Kabwili mpigaji akiingilia shambulizi zuri la winga Salum Kihimbwa.

Dakika ya 59 Mtibwa walimtoa nahodha wao Awadh Juma nafasi yake ikichukuliwa na Japhary Kibaya mabadiliko ambayo yalilenga kuongeza nguvu katika kutafuta bao la kusawazisha.

Yanga muda mwingi wa kipindi cha pili walionekana kucheza soka la kawaida wakijipa uhakika wa kuwa na bao mkononi.

Dakika ya 71 Mtibwa walimtoa Chanongo nafasi yake ikichukuliwa na Ally Makarani pia dakika tano baadaye wakimtoa Kihimbwa nafasi ikichukuliwa na Omary Sultan.

Mabadiliko hayo yaliinufaisha Mtibwa na kuongeza nguvu katika kulishambulia kwa nguvu lango la yanga.

Dakika ya pili ya nyongeza Mtibwa walifanikiwa kupata bao la kusawazisha likifungwa na beki wa kulia Kibwana Shomari kwa shuti kali na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuufanya mchezo huo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

kwenye hatua hiyo Mtibwa wakaibuka washindi kwa kukwamisha nne kupitia kwa Sultani Omar, Dickson Job, Jaffar Kibaya na Kibwana Shomari, huku Abduhalim Humud 'Gaucho' akikosa mbele ya kipa Kabwili, ilihali Yanga ikzipata kupitia Paul Godfrey na Mapinduzi Balama ndio waliokwamisha kimiani, wakati ya Kelvin Yondani iligonga mwamba na ile ya AbdulAziz Makame ikipaa juu.

Mtibwa hii itakuwa fainali yao ya sita katika Mapinduzi, baada ya kutinga 2007, 2008, 2010 waliobeba taji, 2015 na 2016 ambazo mara zote ilipoteza.

Chanzo: mwananchi.co.tz