Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yalazimisha sare Mbeya City

95398 Pic+yanga Yanga yalazimisha sare Mbeya City

Tue, 11 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji Benard Morrison ameinusuru sherehe ya miaka 85, ya Yanga baada ya kufunga bao akisaidia timu yake kupata sare 1-1 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mashabiki wa Yanga walilazimika kusubiri hadi dakika 75, wakati Morrison alifunga bao la kusawazisha akiunganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdul. Mbeya City ilipata bao la kuongoza mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya beki wa Yanga, Lamine Moro kujifunga mwenyewe wakati akijaribu kuokoa mpira. Matokeo hayo yanaifanya Yanga kubaki katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 38, wakati Simba wakiongoza ligi kwa pointi 53, huku Azam ikiwa ya pili kwa pointi 44. Katika mchezo huo Yanga watajilaumu wenyewe kwani pamoja na kutawala mechi hiyo, lakini washambuliaji wake walishindwa kutumia nafasi kufunga. Kocha wa Mbeya City, Amri Said aliingia katika mchezo huo na mfumo wa 4-5-1 akijilinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza, mfumo uliowapa wakati mgumu Yanga katika eneo la kati. Mshambuliaji wa Mbeya City, Abasirimu Chidiebere alikuwa chini ya ulinzi mkali wa mabeki wa Yanga, Kelvin Yondani pamoja na Lamine Moro. Washambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi, David Molinga pamoja na Morrison walishindwa kutumia nafasi kadhaa walizopata huku kipa wa Mbeya City, Haroun Mandanda akiwa kikwazo kwao. Dakika 40 Mbeya City walifanya shambulizi la kushtukiza baadaya kiungo Seleman Ibrahimu kupiga pasi kwa Chidiebere ambaye alipenyeza kwa Rehan Kibingu aliyepiga krosi, lakini mpira huo uliokolewa na beki wa Yanga, Moro. Dakika hiyo hiyo Mbeya City walipata goli baada ya Yanga kuanzisha mpira mfupi uliodakwa na Chidiebere ambaye alipiga pasi kwa Rehan Kibingu aliyepiga krosi finyu na beki wa Lamine Moro aliugusa mpita huo na kwenda wavuni na kumfanya kipa wake Metacha Mnata asijue nini cha kufanya. KOCHA YANGA MZOZO Kocha wa Yanga, Luc Eymael katika mchezo huu alionekana kuzozana mara kwa mara na mwamuzi wa kati Martin Saanya. Kocha huyo alionekana kufokafoka hali ambayo ilimfanya mwamuzi msaidizi wa mezani Isihaka Mwalile mara kadhaa kujaribu kumtuliza kocha huyo. Katika kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko katika eneo la kiungo kwa kumtoa Said Makapu na kuingia Papy Tshishimbi kuweka nguvu katika eneo hilo. Yanga ilionekana kuingia kwa kushambulia zaidi baada ya kutengeneza mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la Mbeya City. Dakika 49 Ditram Nchimbi alifanya shambulizi nje ya 18 baada ya kupiga shuti kali lakini hata hivyo lilitoka nje. Dakika 51 Nchimbi alikimbia akitokea upande wa kulia na kupiga krosi ndani ya boksi na kukutana na Morrison ambaye alipiga shuti na kupanguliwa kwa umakini na kipa wa Mbeya City, Haroun Mandanda na kuwa kona isiyokuwa na faida. Yanga walionekana wakitumia zaidi upande wa kulia aliokuwa anacheza Juma Abdul na Nchimbi kupeleka mashambulizi na yalikuwa yanaonekana kuleta matatizo upande wa lango la Mbeya City. Licha ya kuingia Papy Tshishimbi katika eneo la kiungo bado Yanga walikuwa wakipata tabu mbele ya viungo Seleman Ibrahimu, Ally Nassoro na Emmanuel Memba. Dakika 59 mashabiki wa Yanga walipigwa butwaa baada ya winga wa Morrison kumchambua vizuri beki wa Mbeya City, Keneth Kunambi na kuingia ndani ya boksi na kufanyiwa madhambi na Rolland Msonjo na kudondoka chini, lakini muamuzi wa kati Martin Saanya alionyesha ishara ya mikono kukataa na kelele za mashabikinzilisilika. Dakika 62 Ditram Nchimbi alipewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Peter Mapunda wakati huohuo Yanga ikifanya mabadiliko ya kutoka Molinga na kuingia Tariq Seif. Kipa wa Mbeya City, Haroun Mandanda alipewa kadi ya njano na mwamuzi Martin Saanya baada ya kudaka mpira dakika 66 na kuigiza kuumia. Mbeya City ilifanya mabadiliko ya kiungo dakika 73 kwa kumtoa Seleman Ibrahimu na kuingia Samson Madereka huku upande wa Yanga wakimtoa Nchimbi na kuingia Deus Kaseke.

Mbinu ya Yanga kutumia upande wa kulia kupeleka mashambulizi ilizaa matunda dakika 75 baada ya beki wa kulia, Juma Abdul kupiga krosi ya juj na kuingia moja kwa moja ndani ya boksi na kukutana na Morrison aliyeunganisha krosi hiyo kwa kichwa na kwenda moja kwa moja wavuni. Uwezo wa winga huyo ulionekana kuwa mkubwa baada ya kubadilishana na Kaseke kutoka kucheza upande wa kushoto na kuja kulia katika dakika 82 aliwachomoka mabeki wa Mbeya City na kuingia ndani ya boksi na kufyatuka shuti lililowagonga mabeki wa timu hiyo na kuwa kona isiyokuwa na faida. Mbeya City walifanya mabadiliko mengine dakika 88 kumtoa Peter Mapunda na kuingia Mohamed Mussa. Yanga: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Said Makapu, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima, David Molinga, Balama Mapinduzi, Bernard Morrison Mbeya City: Haroun Mandanda, Keneth Kunambi, Hassan Mwasapili, Ibrahim Ndunguli, Rolland Msonjo, Emmanuel Memba, Rehani Kibingu, Ally Nassoro, Abasirim Chidiebele, Pater Mapunda, Seleman Ibrahimu

Chanzo: mwananchi.co.tz