Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yajiuliza, Azam yafanya maamuzi

Yangasc Kosi Yanga SC

Thu, 13 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uongozi wa Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga umesema utatoa taarifa rasmi kuhusiana na ushiriki wao katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kagame Cup yaliyopangwa kufanyika kuanzia Julai 6 hadi 22, mwaka huu hapa nchini.

Mpaka jana Yanga ilikuwa haijathibitisha sambamba na Azam FC, kushiriki michuano hiyo itakayofanyika kwenye viwanja vya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema uongozi wa klabu hiyo utaweka hadharani uamuzi waliofikia kuhusu mashindano hayo hivi karibuni ili kila mwanachama afahamu mustakabali wao.

"Uongozi unajiandaa kutoa tamko la klabu, wanachama na mashabiki watulie, tutatoa tamko letu rasmi kuhusiana na mashindano haya," alisema kwa kifupi Kamwe.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zacharia 'Zaka Zakazi' aliliambia gazeti hili timu yao haitashiriki mashindano hayo kwa sababu ya muda uliopangwa kutokuwa rafiki.

Zaka alisema wachezaji wao wameenda mapumziko na watarejea rasmi kuanza maandalizi ya msimu mpya Julai 4, mwaka huu.

"Ili timu iweze kukuonyesha kitu inahitaji kufanya mazoezi ya pre season kwa muda wa wiki sita, sasa sisi tutaanza kambi siku mbili kabla ya kuanza mashindano, na hapo wachezaji wanarejea wengine wakiwa na vitambi," Zaka alisema.

Hata hivyo aliongeza endapo ratiba ya mashindano hayo itabadilika na kuanza Agosti, Azam FC itakuwa tayari kushiriki michuano hiyo.

Timu nyingine kutoka Bara zitakazoshiriki michuano hiyo ni Simba na Coastal Union wakati TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Red Arrows (Zambia) na Nyasa Big Bullets ya Malawi ni timu waalikwa.

APR ya Rwanda, El Merreikh, Hai El Wahdi, El Hilal (Sudan), Gor Mahia (Kenya), SC Villa (Uganda), El Merreikh Bentiu (Sudan Kusini) na JKU ya Zanzibar, pia zimetajwa kushiriki michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Express ya Uganda ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kuwafunga Nyasa Big Bullets bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam mwaka, 2021.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live